Polisi mkoani Ruvuma inawashikilia waendesha bodaboda 20 Manispaa ya
Songea wanaodaiwa kumshambulia askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ) Kikosi cha 411 KJ Ruhuwiko, kwa kupiga mawe gari alilokuwa
akiendesha baada ya kumgonga mtembea kwa miguu.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zubeir Mwombeji alisema tukio hilo lilitokea
Machi 24 saa 3.00 usiku maeneo ya Shule ya Msingi Mfaranyaki, karibu na
Kituo Kikuu cha Polisi Songea Mjini.
Mwombeji alimtaja mwanajeshi
huyo aliyejeruhiwa kwa kushambuliwa na waendesha bodaboda kuwa ni Luten
Samweli Nginila (32), ambaye amelazwa Hospitali ya Rufani Mkoa.
Alisema
Luteni Nginila alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili na kupoteza
fahamu baada ya kushambuliwa na waendesha bodaboda, ambao walivunja kwa
mawe vioo vya gari alilokuwa akiendesha.
Aliendelea kuwa chanzo
cha tukio hilo, inadaiwa kutokea ajali maeneo ya majengo ambako askari
huyo alikuwa akiendesha gari aina ya Nissan XTRAIL akitokea Bar ya
Ramour .
Alisema alipofika eneo la majengo, Bahati Mbero
alikatisha ghafla barabarani hivyo askari huyo kushindwa kumudu gari na
kusababisha ajali.
Kufuatia hali hiyo, waendesha bodaboda
waliokuwa karibu walikusanyika kwa lengo la kumshambulia, hali
iliyomlazimu kuwasha gari kukimbia ili kuokoa maisha.
Hata
hivyo, bodaboda hao walimkimbiza na alipofika Shule ya Msingi Mfaranyaki
tairi la gari lake lilichomoka, hivyo walimzingira na kumshushia kipigo
wakiwamo abiria watatu aliokuwa nao.
Mwombeji aliwataja
waliokuwamo ndani ya gari hilo kuwa ni Kaumbya Kateka (24) mkazi wa
Majengo, Joyce Edson (24) mkazi wa Mpambalyoto na Jackline Mwita (22)
mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Peramiho. Alisema katika vurugu hizo
baadhi ya vitu vilipotea ambavyo ni mali ya askari huyo.
Vitu vilivyopotea ni simu mbili za mkononi, pochi ambayo ilikuwa imehifadhi vitambulisho mbalimbali na Sh120,00.
Alisema wanaendelea kuwabaini wengine waliohusika, taratibu za kuwafikisha mahakamani zitafuata.
No comments:
Post a Comment