Wananchi wilayani Kiteto mkoani Manyara wamejiandaa kumpokea kwa mabango Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ili kutoa ujumbe wa kuwakataa baadhi ya viongozi wa wilaya kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi.
Miongoni mwa viongozi wanaotajwa kuwamo katika ujumbe huo ni Mkuu wa Wilaya Kanali Samweli Nzoka, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Bosco Ndunguru,Katibu Tawala (DAS) Nicodemus John pamoja na kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD) George Katabazi.
Hata hivyo DC Nzoka amepiga marufuku mwananchi yeyote kuandaa bango lolote katika ziara hiyo ya Waziri Mkuu inayotarajiwa kufanyika Februari 29 mwaka huu.
Akizungumza katika kikao cha baraza la Madiwani jana,Nzoka alisema hataruhusu kuandaliwa wala kuonyeshwa mabango hayo kwani ni ishara ya vurugu na uvunjifu wa amani.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema anazo taarifa za kuwapo watu walioandaliwa kutoka wilaya na mikoa ya jirani kwenda Kiteto kuzomea baadhi ya viongozi wa Wilaya katika ziara hiyo.
Katika ziara hiyo, Majaliwa atakutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani, wakuu wa idara na viongozi wa mila wa jamii ya wafugaji
Waziri mkuu anategemewa kutoa suluhisho la mgogoro wa ardhi kati ya wakulima na wafugaji uliodumu kwa muda mrefu na kusababisha mauaji.
No comments:
Post a Comment