Timu ya soka ya Singida United yapanda daraja - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 22 February 2016

Timu ya soka ya Singida United yapanda daraja

Singida United
TIMU ya soka ya Singida United ya mjini Singida, hatimaye imekata tiketi ya kucheza ligi daraja la kwanza mwaka huu baada ya kuifunga bila huruma timu ya Abajalo F.C. ya wilayani Igunga, Mkoani Tabora kwa jumla ya magoli mawili bila majibu.Katika mchezo huo mkali na wa kusisimua,ulifanyika katika uwanja wa kumbukumbu ya michezo wa Namfua mjini Singida na pia kuhudhuriwa na wapenzi na washabiki wa soka wachache.
Singida United
Wachezaji wa timu ya Abajalo na Singida United wakigombea mpira kwenye eneo la hatari la lango la Abajalo kwenye uwanja wa Namfua kwenye mchezo huo wa ligi daraja la pili taifa, Singida United ilitoka kifua mbele baada ya kuigaragaza Abajalo magoli 2-0.
Hata hivyo inadaiwa kuwa mchezo huo uliokuwa na mahudhurio hafifu,kwa kiasi kikubwa yaliathiri na mchezo  kati ya Yanga na Simba za jijini Dar-es-salaam.Singida United iliyocheza ligi kuu mwaka 2000 na kushuka daraja miaka miwili baadaye,ililazimika kusubiri hadi dakika ya 50 ndipo ilipopata goli la kwanza kupitia kwa Hassani Mseka.Hata hivyo Mseka alifunga goli hilo baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa timu ya Abajalo na kuachia shuti kali lililomshinda kipa,Alli Mashaka.
Timu ya Abajalo ilianza kulishambulia mfululizo lango la Singida baada ya kufungwa goli hilo la kuongoza,huku ikijikuta ikikosa magoli ya wazi katika dakika ya 69,73 pamoja na 78,kutokana na washambuliaji wake kutokuwa makini pindi walipokuwa wanalikaribia lango la wapinzani wao.
Singida United
Baadhi ya askari polisi wa mjini Singida, wakimwokoa mshika kibendera namba moja kupigwa na wachezaji wa Abajalo ya mkoa wa Tabora. Abajalo walipandwa na hasira baada ya kufungwa goli la kwanza na Singida United.Hata hivyo timu ya Singida United ilifanya shambulizi la kushitukiza katika dakika ya 82 na kufanikiwa kufunga goli la pili kupitia kwa Davidi Gregory aliyetokea benchi.


Songa Jared wa Singida United aliyeng’ara katika mchezo huo aliwalamba chenga walinzi watatu wa Abajalo na kutoa pasi safi kwa Gregory ambaye alisukumia mpira huo upande wa kushoto wa lango la Abajalo huku kipa Mashaka akijikuta akilamba vumbi upande wa kulia.
Katika dakika ya 81,mwamuzi wa mchezo huo kutoka mjini Dodoma, Doto Ibrahimu alimtoa nje ya uwanja kwa kadi nyekundu Ramadhani Mrisho wa Abajalo,baada ya kumchezea vibaya Yusuph Kagoma wa Singida United.Wakati huo huo, Singida United imeanza mazoezi makali kwa ajili ya kwenda kuilambisha timu ya Simba ya jijini Da-es-salaam feb,28,mwaka huu zitakapokutana kwenye mchezo wa FA.
Singida United
Mwamuzi wa mchezo kati ya timu za soka za Singida United ya mjini Singida na Abajalo ya wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora, Doto Ibrahimu kutoka Dodoma mjini, akimtoa nje kwa kadi nyekundu mchezaji wa Abajalo Ramadhan Mrisho kwa kumchezea rafu mbaya Yusuph Kagoma wa Singida United.
Singida United
Timu ya soka ya Abajalo F.C. kutoka wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora iliyofungwa goli 2-0 na Singida United kwenye uwanja wa Namfua mjini Singida kwa ushindi huo, Singida United imekata tiketi ya kushiriki ligi daraja la kwanza mwaka huu.
Singida United
Baadhi ya wapenzi wa soka wa mjini Singida, waliohudhuria pambano kali na la kusisimua kati ya Singida United na Abajalo ya Igunga mkoani Tabora.
Post a Comment