Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Singida umetoa msaada zaidi ya
shilingi 11.2 bilioni kwa ajili ya kunusuru kaya masikini 40,218 kati ya
Septemba 2014 na Desemba mwaka jana.
Hayo
yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Manyoni na Mbunge Viti Maalum, Fatma
Toufiq, wakati akifungua kikao cha siku moja cha kuwajengea uwezo
waratibu, madiwani na wadau wengine wa mpango wa TASAF III, ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Mkuu wa
wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Fatma Toufiq, akizungumza kwenye
ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waratibu wa TASAF
halmashauri mpya ya Itigi. Kulia ni Kaimu Katibu Tawala mkoa wa Singida,
Boniface Temba na wa kwanza kushoto, ni Mkurugenzi mtendaji wa
halmashauri ya Itigi.
Alisema
kaya hizo maskini zilizonufaika na msaada huo,zipo kwenye Vijiji 2,726
na kati ya Vijiji hivyo, Vijiji 30 ni vya Halmashauri ya Itigi ambayo
ina Vijiji 39.
Akifafanua,
Fatma alisema wilaya ya Ikungi imepewa zaidi ya shilingi Bilioni Tatu,
Iramba 1.9 bilioni, wilaya ya Singida Bilioni 2, Manispaa ya Singida
Bilioni moja na Ofisi ya katibu tawala mkoa milioni 104.5.
Mkuu huyo
wa wilaya,alisema lengo la msaada huo, ni kuzijengea uwezo na
kuziwezesha kaya hizo maskini kuongeza kipato, ili ziweze kumudu
kugharamia mahitaji yao muhimu na masomo ya watoto wao.
Mratibu
TASAF mkoa wa Singida, Patrick Kasango, akitoa nasaha zake kwenye
ufunguzi wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo waratibu wa TASAF wa
halmashauri mpya ya Itigi wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Katika
hatua nyingine, DC huyo alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana
kutokana na msaada huo, ni kuongezeka kwa mahudhurio ya wanafunzi wa
shule za msingi na sekondari na pia ongezeko la wanafunzi
walioandikishwa mwaka jana.
“Pia
msaada huo, umepunguza vifo vya akina mama wajawazito na vifo vya watoto
wenye umri wa chini ya miaka 5 kwa mwaka jana. Vifo hivyo vimepungua
ikilinganishwa na mwaka juzi, kutokana na akina mama wajawazito
kuhudhuria kliniki ikiwa ni sharti mojawapo la mpango huo,” alisema.
Aidha,
Mkuu huyo wa Wilaya, amewataka viongozi wa watendaji kuendelea
kuwashauri na kuwahamasisha wazitumie fedha hizo kwa malengo
yaliyokusudiwa, ili kuleta matokeo chanya na kuondoka kwenye umaskini.
Mratibu
wa TASAF halmashauri ya wilaya ya Ikungi na manispaa ya Singida, Majuto
Kawambwa, akitoa mada yake iliyohusu majukumu ya waratibu wa TASAF ngazi
ya halmashauri na wadau wengine wa mfuko huo,juzi kwenye semina ya siku
moja iliyohudhuriwa na wadau TASAF halmashauri wilaya Itigi.
Kwa
upande wake Mratibu wa TASAF mkoa wa Singida,Patrick Kasango, alisema
watendaji wa vijiji na kata hawaruhusiwi kujihusisha na shughuli ya
ulipaji wa fedha za TASAF kwa walengwa.
“Katika
mpango huu wa TASAF III, watendaji wamepewa jukumu la kusimamia tu zoezi
la utoaji wa msaada wa fedha za kunusuru kaya maskini, na si
vinginevyo. Aidha, hairuhusiwi fedha za walengwa kuchukuliwa na mtu
mwingine, mlengwa asiohudhuria siku ya kutoa msaada, fedha zake
zitarudishwa na zitalipwa awamu itakayofuata,” alifafanua Kasango.
Mkuu wa
wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida na mbunge viti maalumu Dodoma, Fatma
Toufiq (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wataribu wa TASAF
mkoa na halmashauri wilaya ya Itigi.Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi
mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Itigi, Msafiri Abdalah na
anayefuatia ni Mwenyekiti wa halmashauri Itigi, Alli Minja.
No comments:
Post a Comment