SHULE 10 BORA,SHULE 10 ZA MWISHO,NA ALIYEFAULU KULIKO WOTE MATOKEO YA KIDATO CHA NNE. - LEKULE

Breaking

18 Feb 2016

SHULE 10 BORA,SHULE 10 ZA MWISHO,NA ALIYEFAULU KULIKO WOTE MATOKEO YA KIDATO CHA NNE.


Baraza la mitihani Tanzania limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2015 yanayoonesha kiwango cha ufaulu kushuka kwa asilimia 0.80.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt Charles Msonde amesema kuwa jumla watahiniwa 272,947 sawa na 67.53% ya watahiniwa wote waliofanya mtihani wa kidato cha nne 2015 wamefaulu tofauti na mwaka 2014 ambapo ufaulu ulikuwa 68.33%.

Msonde amesema kwa upande wa watahiniwa wa shule, waliofaulu ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 ya waliofanya mtihani, wasichana wakiwa 11,125 (64.84) na wavulana wakiwa 124,871 (71.09).

Amesema kwa upande wa watahiniwa wa shule, ufaulu umeshuka kwa asilimia 1.85 ikilinganishwa na mwaka 2014.

Aidha kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, Dkt Msonde amesema watahiniwa 31,951 sawa na asilimia 64.80 wamefaulu ikilinganishwa na watahiniwa 29,162 (61.12) waliofaulu mwaka 2014.

Kwa upade wa ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule, Msonde amesema waliopata daraja la kwanza ni 9,816 sawa na asilimia 2.77, daraja la pili ni 31,986 sawa na asilimia 9.01, daraja la tatu ni 48,127 sawa na asilimia 13.56.

Aidha waliopata daraja la nne ni 240,996 sawa na asilimia 67.91 na waliopata daraja la sifuri (waliofeli) ni 113,489 sawa na asilimia 32.09.

Watahiniwa waliopata ufaulu mzuri wa kati ya daraja la kwanza hadi la tatu ni 94,941 sawa na asilimia 24.73 wavulana wakiwa 56,603 sawa na 29.99 na wasichana 38,338 sawa na asilimia 19.63.

Amesema kwa upande wa ufaulu wa masomo kwa watahiniwa wa shule, ufaulu wa juu kabisa ni wa somo la Kiswahili ambapo asilimia 77.63 wamefaulu huku ufaulu wa chini kabisa ukiwa ni wa somo la Basic Mathematics ambapo asilimia 16.76 wamefaulu.

Baraza hilo limezuia matokeo ya watahiniwa 121 kutokana na sababu za kiafya na watahiniwa hao wataruhusiwa kufanya mitihani ambayo hawakuifanya katika mtihani wa kidato cha nne, mwaka 2016.

Aidha baraza hilo limefuta matokeo ya watahiniwa 87 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani ambapo kati yao 25 ni wa kujitengemea na 52 ni watahiniwa wa shule wakati 10 ni wa mtihani wa maarifa (QT)

Amezitaja shule 10 zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilizofanya vizuri zaidi kuwa ni Kaizerege ya mkoani Kagera, Alliance Girls ya Mwanza, St. Francis Girls ya Mbeya, Canossa ya Dar es salaam, Marian Boys ya Pwani, Alliance Rock Army ya Mwanza, Feza Girls Dar es salaam, Feza Boys ya Dar es salaam na Uru Seminary ya Kilimanjaro.

Shule 10 zilizofanya vibaya zaidi kwa watainiwa zaidi ya 40 ni pamoja na Pande ya mkoani Lindi, Igawa ya Morogoro, Korona ya Arusha, Sofi ya Morogoro, Kurui ya mkoani Pwani, Patema ya Tanga, Saviak ya Dar es salaam, Gubali ya Dodoma, Kichangani ya Morogoro na Malinyi ya Morogoro.

Kwa upande wa watahiniwa, Dkt Msonde amesema kati ya watahiniwa 10 waliofanya vizuri zaidi, wanne na wasichana na sita ni wavulana.

Mwanafunzi aliyeongoza ni msichana Butogwa Charles Shija wa Canossa, akifuatiwa na msichana mwingine Congcong Wang wa Feza Girls na wa tatu ni mvulana Innocent Lawrence wa Feza Boys.

Wengine ni Dominick Marco Aidano wa Msolwa, Sang'udi E Sang'udi wa Ilboru, Asteria Herbert Chilambo waCanossa, Belinda Jackson Magere wa Canossa, Humfrey Martine Kimanya wa Msolwa, Bright B Mwang'onda wa Marian Boys na wa 10 ni Erick R Mwang'ingo wa Marian Boys.

Matokeo hayo yamepangwa katika mfumo wa madaraja (Division) badala ya ule wa wasatani wa alama (GPA) kama ambavyo iliagizwa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi hivi karibuni.
 

No comments: