SERIKALI YAKEMEA UVAMIZI WA MIUNDOMBINU - LEKULE

Breaking

18 Feb 2016

SERIKALI YAKEMEA UVAMIZI WA MIUNDOMBINU



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kampuni ya Simu (TTCL), kanda ya ziwa Peter Kuguru kuhusu nguzo za alama zinazoonyesha sehemu ulikopita mkongo wa taifa.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akipata maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa Mitambo ya Mawasiliano ya TTCL mjini Shinyanga.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akimuonesha moja ya mifuko inayotumika kuhifadhi barua  Meneja wa Posta mkoa wa Shinyanga Eugenia Punjira, alipokagua utendaji wa shirika hilo.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (katikati) akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Stesheni ya Reli Shinyanga Bw. Baruani Issa (kulia) kuhusu kuanza kutumia jengo la kuhifadhia mizigo (ICD) katika stesheni hiyo.

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiongea na sehemu ya wafanyakazi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) mkoani Shinyanga.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa wafanyakazi wa sekta za ujenzi, uchukuzi na mawasiliano kuhusu kufanya kazi kwa umoja na kutekeleza malengo waliyokubaliana ili kukuza uchumi wa taasisi hizo na kuleta tija.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiwa amesimama juu ya reli ya kati mjini Shinyanga, mbele ni nyumba ya makazi iliyojengwa juu ya reli hiyo na kuizuia.
Serikali imekemea vikali vitendo vya baadhi ya wananchi kujenga katika maeneo yenye miundombinu ya barabara na reli na hivyo kusababisha usumbufu, hujuma na uharibifu wa mali za umma.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameyasema hayo wakati akikagua sehemu ya njia ya reli ya kati, mjini Shinyanga na kukuta nyumba iliyojengwa na kuzuia reli. BOFYA HAPA KUSOMA ZAIDI
“Kazi ya Serikali ni kujenga Miundombinu na kazi ya wananchi ni kulinda Miundombinu, Mkuu wa mkoa hakikisha nyumba hii inabomolewa haraka na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wote waliohusika na hujuma hii”, amesema Prof. Mbarawa.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bw. Ally Rufunga amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa Serikali mkoani humo itatekeleza maelekezo yake na kuhakikisha miundominu ya barabara, reli na mawasiliano inalindwa wakati wote.
Waziri Prof. Mbarawa amewahakikishia watumishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), kuwa Serikali iko katika hatua za kuunganisha TRL na Kampuni Miliki ya Rasilimali za Reli (RAHCO) ili kuongeza ufanisi wa shirika hilo na kuwataka kuanza kutumia jengo la Hifadhi ya Mizigo (ICD)iliyojengwa na RAHCO ambalo haijatumika kwa takribani miaka mitatu sasa.
Amekemea vitendo vya uvivu na hujuma vinavyofanywa na watumishi wasio waaminifu vya kuiba mafuta na kuangusha mabehewa na hivyo kulisababishia hasara Shirika hilo.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema tayari TRL imeaanza kusafirisha makontena kutoka bandari hadi ubungo ambapo kwa sasa takribani makontena mia moja yanatoka bandarini na kusafirishwa kwa njia ya Reli hatua ambayo itahuisha utendaji wa Shirika hilo.
Waziri Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa TRL kutoa ushirikiano kwa Uongozi mpya ili kuwezesha kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Tutaendelea kusafisha TRL ili lifanye kazi kwa faida, mchezo wa kuangusha mabehewa na kuiba mafuta  ufike mwisho, lazima tuchunguze na sheria ichukue mkondo wake kwa wote waliofanya vitendo hivyo”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Stesheni ya Shinyanga Bw.Baruani Issa ameiomba Serikali kutumia usafiri wa reli kusafirisha mizigo mingi ili kufufua Shirika hilo na kulinda miundombinu ya barabara.
Waziri Prof. Mbarawa amewahakikishia watumishi wa TRL kuwa mpango wa kujenga reli ya kisasa Standard Gauge upo na utatekelezwa kwa awamu ili kuwezesha reli hiyo kubeba mzigo mkubwa na kuongeza mapato kwa Shirika na kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Mbarawa yupo katika ziara ya kukagua miundombinu ya ujenzi, uchukuzi na mawasiliano katika mikoa ya kanda ya ziwa ambapo amewataka wasimamizi na wafanyakazi wa TANROADS, TEMESA, TBA, SUMATRA, TRL,TAA,TMA,TTCL na POSTA kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kufikia lengo la kuwajengea watanzania miundombinu itakayowafikisha kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

No comments: