Mwenyekiti
wa tume ya uchaguzi hapa nchini Mheshimiwa Jaji Damian Lubuva
amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kuwa tume hiyo ipo huru na haijawahi kuingiliwa kimaamuzi na
Rais wala kiongozi yoyote.
Jaji
Lubuva amesema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam mara baada ya
kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ambapo alikuwa akimpa
taarifa juu ya yaliyojiri katika kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki
kilichofanyika Mjini Kampala, Uganda na kujadili kuhusu uchaguzi Mkuu wa
Uganda unaotarajiwa kufanyika tarehe 18 mwezi huu.
Amesema
katika kikao hicho ambacho yeye alikuwa mwenyekiti, wamezungumzia
umuhimu wa tume ya uchaguzi kuwa huru huku wakichukulia mfano wa
Tanzania ambayo imetoka katika uchaguzi mkuu miezi michache iliyopita.
Jaji
Lubuva amefafanua kuwa tume ya uchaguzi inapaswa kuwa huru katika
maamuzi yake na kwamba jambo hili limekuwa likifanyika wakati wote hapa
nchini.
Amebainisha kuwa wanaosema Rais anapaswa kuingilia kati masuala ya uchaguzi iwe Tanzania bara ama Zanzibar wanafanya makosa, kwani kwa namna yoyote Rais hana mamlaka hayo na hivyo hawezi kuingilia maamuzi ya tume hizo
“Unaposikia
kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano aingilie hilo suala la uchaguzi wa
Zanzibar, yeye kwa kweli hana mamlaka kabisa. Pili ni kama kujikanganya,
huku unasema tuwe na tume huru isiyoingiliwa halafu huku unasema
aingilie kati maamuzi ya tume” alisema Jaji Lubuva
Jaji
Lubuva amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kikatiba hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya tume ya uchaguzi ya
Zanzibar na hata huku bara pia hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya
tume.
Mwenyekiti
huyo wa tume ya uchaguzi amewasihi Watanzania kuwa uchaguzi umekwisha,
na kuwaomba waungane na viongozi waliochaguliwa kuchapa kazi ili
kujiletea maendeleo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam.
01 Februari, 2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akimkaribisha Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Ramadhan Kailima Ikulu Jijini
Dar es Salaam.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji
Damian Lubuva Ikulu Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa
Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Ramadhan Kailima Februari 01,2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiagana na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Damian Lubuva
Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo
No comments:
Post a Comment