Polisi mkoani Katavi inamshikilia Mratibu Elimu Kata ya Katuma wilayani Mpanda, Mohamed Muna (59) kwa tuhuma za kumchoma kisu na kumuua mkazi wa kitongoji cha Misheni, Gidison Vincent (32), anayedaiwa kuwa mgoni wake.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alimuua Gidison baada ya kumfumania ndani ya nyumba yake akifanya mapenzi na mkewe, Ester Kasansa ‘Chuki’ (36).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari akithibitisha alisema mkasa huo ulitokea Januari 27, mwaka huu saa 02:30 usiku, katika Kitongoji cha Mashineni, Kata ya Katuma wilayani Mpanda.
“Usiku huo wa tukio, mtuhumiwa alimkuta Gidison (sasa marehemu) akiwa ndani ya nyumba yake akifanya mapenzi na mke wake aitwaye Ester, ndipo alipogonga mlango wa chumbani na mgoni wake (marehemu) kutoka nje na kuanza kupambana naye, ambapo mtuhumiwa alimchoma kisu kifuani na kukimbia,” Kidavashari alisema.
Kwa mujibu wa Kidavashari, chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi na mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa awali kukamilika ili kujibu tuhuma inayomkabili.
No comments:
Post a Comment