KILIO
cha ukosefu wa fedha za kuonesha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge la
Tanzania kupitia Shirika la Utangazaji nchini (TBC) ambacho kimekuwa
kikitolewa na serikali, sasa kimepata ufumbuzi.
Mfuko
wa Vyombo vya Habari nchini (TMF) umeeleza kwamba upo tayari kutoa
fedha zinazohitajika ili kuhakikisha haki ya Mtanzania kupata habari
kupitia TBC haiingiliwi wala kubughudhiwa kwa hoja yoyote.
Endapo
serikali itakubali ombo hilo, wananchi wataendelea kunufaika na vikao
vya moja kwa moja vya bunge tofauti na pendekezo la serikali la kunakili
baadhi ya sehemu na kisha kuoneshwa usiku.
Ernest
Sungura, Mkurugenzi Mtendaji wa TMF leo jijini Dar es Salaam amewaeleza
wahariri wa habari na serikali kupitia mwakilishi wake Assah Mwambene
ambaye ni Mkurugenzi wa Habari Maelezo kwamba, taasisi hiyo imejipanga
kusimamia na kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata matangazo ya moja
kwa moja kutoka bungeni kupitia TBC kwa kuyagharamia.
Sungura
amesema kwamba miongoni mwa malengo ya mfuko huo ni pamoja na kuleta
mabadiliko katika tasnia ya habari pia kuhakikisha wananchi wanapata
taarifa.
Januari
mwaka huu, Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya serikali kusitisha matangazo ya
moja kwa moja ya bunge kupitia TBC.
Miongoni
mwa sababu alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa ya Sh.
4.2 bilioni zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa
moja kwa mwaka pia watumishi wa serikali kushabikia bunge badala ya
kuendelea na kazi ofisini.
Hatua
ya serikali kusitisha matangazo hayo iliibua mjadala mkubwa bungeni
huku Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) akilitaka bunge
kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya serikali.
Nje
ya bunge mjadala huo uliendelea bila kupatikana kwa ufumbuzi ambapo TMF
imedhamiria kugharamia matangazo hayo ili kuruhusu wananchi kuendelea
kupata matangazo hayo kupitia TBC.
Katika
mkutano huo, Mwambene amesema kwamba, serikali itafikiria namna ya
kupeleka maombi TMF ya uwezeshwaji katika maandalizi ya miswada miwili
ya sheria za habari ili kupitisha sheria zenye matakwa ya wadau.
Kuhusu
hilo, Sungura amesema taasisi yake iko tayari kuisaidia serikali kwenye
mchakato huo na hata kuitisha kongamano kubwa la wadau.
No comments:
Post a Comment