Mchakato Wa Kura Ya Maoni Ya Katiba Mpya WANUKIA NUKIA - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Tuesday, 16 February 2016

Mchakato Wa Kura Ya Maoni Ya Katiba Mpya WANUKIA NUKIAMwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, amesema mchakato wa Kura ya Maoni ya Katiba mpya umeanza baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.

Kauli hiyo ya Jaji Lubuva imekuja wakati wadau wa siasa nchini wakimtaka Rais Dk. John Magufuli, kutoendelea na Kura ya maoni badala yake mchakato wa Katiba mpya urudi nyuma baadhi ya mambo yaliyo kwenye Katiba iliyopendekezwa yarekebishwe.

Itakumbukwa kuwa mchakato wa Katiba mpya uliingia dosari baada ya baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupinga mfumo wa Serikali Tatu uliokuwa umependekezwa na Tume ya Jaji mstaafu Joseph Warioba, iliyokusanya maoni nchi nzima na matokeo yake kuzaa kundi lililojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Tulikuwa tunangoja tumalize uchaguzi, kama vile ambavyo Mnyamwezi anavyobeba mzigo, unamaliza mmoja unakwenda kwa mwingine. Sasa tumemaliza (uchaguzi mkuu), tunakwenda kwa lingine (Kura ya Maoni),”alisema Jaji Lubuva.

Aliongeza: “Tunaliangalia na kama Tume tutakuja kuwajulisha wananchi hali ikoje, tuliahirisha (Kura ya Maoni) ili tumalize hili (uchaguzi mkuu).”alisema Jaji Lubuva na kuongeza.

“Hili ni suala linalohitaji mambo ya bajeti kubwa na ndiyo tumetoka kwenye uchaguzi na serikali ndiyo inaanza, kwa hiyo ni suala ambalo tunaliangalia na baadaye wananchi watajulishwa,” alisema Jaji mstaafu Lubuva.

Alipoulizwa kuhusu makadirio ya bajeti ya kuendesha kura hiyo ya maoni, Lubuva alisema: “Hilo niulize siku nyingine, sina zaidi ya hapo kwa leo.”

Rais Magufuli alipokuwa akihutubia Bunge la 11 siku ya kulizindua Novemba 20, mwaka jana, alisema serikali yake imepokea kiporo cha mchakato wa Katiba ambao haukukamilika katika awamu iliyomtangulia kutokana na kutokukamilika kwa wakati kwa uandikishaji wapiga kura.

“Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kuthamini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba mpya, Tume ya Marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lililotupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ulivyoainishwa katika Sheria ya Marekebisho ya Katiba,” alisema Rais Magufuli. 

Mbali na muundo wa serikali tatu, baadhi ya mambo ambayo Ukawa walitaka yawe kwenye Katiba mpya ni mamlaka ya Rais kupunguzwa, ushindi wa Rais uwe zaidi ya asilimia 50, Tume huru ya Uchaguzi, matokeo ya Rais kupingwa mahakamani, kuwe na mgombea binafsi, mawaziri wasitokane na wabunge, na muundo mpya wa Bunge la Muungano.

Post a Comment