Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imetoa siku saba kwa mawakili waandamizi wa Serikali kutoa majibu ya kuendelea kusikilizwa kwa kesi ya aliyekuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Vunjo wa TLP, Augustine Mrema .
Januari 18, mwaka huu, mahakama ilimpa siku 12 Mrema kwenda kufanya marekebisho ya maombi yake aliyokuwa amepeleka mahakamani hapo ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge James Mbatia (NCCR Mageuzi).
Akitoa uamuzi huo mbele ya wakili mwandamizi wa Serikali, Omary Kibwana akisaidiana na Glory Efatha, Jaji Benedict Mwingwa alisema kwa siku saba mawakili hao watatakiwa kupeleka majibu ili kesi hiyo iweze kuendelea kusikilizwa.
Jaji alisema Februari 18, mwaka huu ndiyo siku ambayo watasikiliza kesi hiyo baada ya mawakili hao kupeleka majibu mahakamani hapo na Februari 15.
Awali, mawakili hao waliiomba mahakama kupewa muda wa kutosha wa kujibu maombi ya marekebisho hayo ili kesi iweze kuendelea kusikilizwa.
Wakili anayemwakilisha Mbatia, Youngsevia Msuya aliiomba mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo Februari 18 badala ya Februari 15.
Awali, Mrema ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, alifungua kesi hiyo kupinga ushindi wa Mbatia aliyepata kura 60,187 dhidi ya kura 16,617 za Mrema katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini Oktoba 25, mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment