Kwa karibu miaka 30, Gregoire Ahongbonon, fundi wa mitambo kutoka Benin, amewasaidia watu wengi Afrika Magharibi walio na matatizo ya kiakili.Amekuwa akiwatunza kwenye vituo vya makazi vinavyosimamiwa na shirika lake lisilo la kiserikali, Shirika la Mtakatifu Camille. Juu ya yote, amejitolea kukabiliana na tabia ya kuwafungia watu wenye matatizo ya kiakili.
Aime ametoka sasa hivi kutoka kwenye chumba chake. Anatembea aste aste, vifundo vyake vya mguu vikiwa vimefungwa kwa vyuma.
Kisa hiki kinatokea katika nyumba ndogo katika mji wa Calavi, viungani mwa mji wa Cotonou, mji mkuu wa Benin. Aime, 24, ana matatizo ya kiakili na kakake mkubwa na dadake wamekuwa wakimtunza kadiri ya uwezo wao.
“Ilitulazimu kumfungia kwa sababu yeye husumbua watu na huwa wanakuja hapa kulalamika,” anasema kakake, Rosinos.
“Wakati mwingine hata hushambulia watu barabarani na kudai wamemwibia kitu. Huwa hakomi kupiga kelele, usiku na mchana. Nimesumbuka sana.”
Familia haingeweza kumudu gharama Aime apokee matibabu katika hospitali pekee ya serikali ya magonjwa ya kiakili, Hospitali ya Umma ya Jacquot, ambapo ada huanzia franka 20,000 za CFA kila mwezi – karibu nusu ya mshahara wa wastani. Badala yake, wenyewe walimpa tiba iliyopendekezwa na hospitali, na baada ya miezi minane hata dawa hizo wakashindwa kuzinunua.
Aime alikuwa ameanza kuwa mtulivu, lakini bila dawa ugonjwa wake ulirejea upesi. Rosinos na dadake, walikuwa wametamauka pale Edmunda alipohudhuria mhadhara wa Gregoire Ahongbonon, aliyekuwa akipinga kutengwa na kubaguliwa kwa watu wenye matatizo ya kiakili.
Baadaye Edmunda alimuomba Ahongbonon ushauri, na Aime sasa anapelekwa kituo kinachosimamiwa na shirika la Mtakatifu Camille eneo la Calavi, ambacho kitawagharimu kiasi kidogo sana cha pesa.
Shirika hilo lina vituo zaidi ya kumi Ivory Coast, Benin, Togo, na Burkina Faso, ambavyo huwahudumia maelfu ya wagonjwa.
Ahongbonon na wafanyakazi wake huwatafuta watu wasio na makao, waliotupwa barabarani na familia zao, na kuwapa makao. Pia husafiri kote Afrika Magharibi wakifuatilia habari za watu wenye matatizo ya kiakili waliofungiwa nyumbani au wanaodhalilishwa na kuteseka vijijini. Wanapompata mtu kama huyo huwa wanamchukua.
"Wagonjwa maradhi ya akili hutazamwa kama watu waliopagawa au waliorogwa,” anasema Ahongbonon.
“Hiyo ndiyo hali Afrika kwa kawaida, lakini hali ni mbaya zaidi Benin, kwa sababu Benin … ndiko kwenye uchawi wa voodoo na hivyo basi imani hii ni kali zaidi.”
Nchini Benin, mtu anapougua, jambo la kwanza kufikiriwa na familia ni kumpeleka kwa mganga wa kiasili au mikutano ya wahubiri wa kiinjilisti wanaodai wanaweza kumponya mtu kupitia maombi
Mjukuu wa Pelagie Agossou, Judikael, alipougua, marafiki zake walimshauri ampeleke kanisa moja akatolewe pepo.
Alikataa ushauri huu, lakini alijaribu mambo mengine mengi, ikiwemo kumtembelea mganga wa kiasili.
Tatizo la Judikael lilikuwa aina ya schizophrenia, na alisikia sauti zikimwambia avue nguo zake na kutoka nje ya nyumba.
"Wakati mmoja, baada ya mtoto wangu kutoroka nyumbani tena, msichana mmoja alinijia na kuniambia kwamba Judikael alikuwa akizurura mjini akiwa na chupi pekee,” anasema Agossou.
"Nilikimbia upesi lakini aliponiona alianza kukimbia… Nilimkimbiza na watu wakaanza kumkimbiza pia, wakifikiria alikuwa mwizi. Mimi naye nilikuwa nikisema kwa sauti ‘Msimdhuru, ni mwanangu.’ Nilikuwa na wasiwasi sana kwamba polisi wangemdhuru wakidhani ni mwizi.”
Alijaribu kumpeleka kliniki ya kibinafsi lakini ilikuwa ghali mno, na ni hapa ambapo aliamua kumtembelea mganga wa kiasili, ambapo alilipa franka 80,000 CFA (£93) na akapewa dawa ambazo hazikufanya kazi.
"Nilimpigia na kuwambia dawa yake haikufanya kazi,” Agossou anasema, “na alijibu, 'Basi acha kumpa.'"
Kuna aina nyingi ya wagonjwa wa kiasili.
Mganga aina ya “bokhonon” huangazia masuala ya kiroho kutambua na kutoa laana, naye “amawato” ni mganga wa dawa za kiasili.
"Mgonjwa anapofika mara ya kwanza, huwa naagua, na kujua iwapo amevunja kaida, alimkosea mtu Fulani au alirogwa,” anasema Nestor Dakowegbe, mmoja wa waganga wa kiasili wanaojulikana sana nchini humo.
"Huwa rahisi kutibu ugonjwa wa kiakili iwapo umetokana na kurogwa au matendo mabaya ya mwathiriwa kwa mababu zake – hapo ni kufidia tu. Lakini iwapo ni wa kurithi au unatokana na jambo la kiasili kama vile kugongwa kichwani, basi huwa vigumu kiasi.”
Nestor Dakowegbe ni mganga wa bokhonon na pia mganga waamawato, kwa hivyo tiba yake huwa na dawa za kiasili, pamoja na maombi kwa miungu pamoja na hatua ambazo mgonjwa anfaa kuchukua. Anajivunia ujuzi ambao familia yake imekuwa nao kwa vizazi vingi, na haoni tishio lolote kutoka kwa tiba za kisayansi.
“Baadhi ya madaktari tayari wananijua. Wanapokuwa na mgonjwa na wanaona dawa ya Mzungu haitafanya kazi, huwa waja kwangu.
„Hili lilifanyika mara nyingi hadi tukawa washirika. Wakati mwingine, mimi pia huwaomba madaktari hawa wa kisasa kunisaidia katika visa vigumu.”
Galbert Ahi, mmoja wa madaktari wa kiakili mjini Benin, na mkurugenzi wa zamani wa hospitali ya Jacquot, ni mmoja wa wanaoamini madaktari wa maradhi ya akili wanaweza kufanya kazi kwa pamoja na waganga wa kiasili.
Ananiambia kuhusu kisa mwanamke mmoja aliyekuwa akitatizwa na msongo wa mawazo, ambaye alimpeleka kwa mganga wa kiasili, na akapona.
"Ilinibidi kunyenyekea sana, daktari aliyebobea na mwenye shahada zake, kwenda kumtafuta mganga kipofu kunisaidia ‘kuona’ tatizo lilikuwa nini,” anasema.
"Baadhi ya waganga husema, tahadhari: „Nyinyi huwa mwatibu lakini sisi huponya”. Na wanamaanisha kuwa baada ya mimi kumtibu mgonjwa, lazima wamalizie kazi. Lazima walainishe kila kitu ili mgonjwa awe mzima tena katika utamaduni wake.”
Gregoire Ahongbonon na wasiwasi kuhusu mpangilio kama huo.
"Mtazamo ambao tunao Afrika ni kwamba waganga ni bora kuliko madaktari wa kawaida katika kutibu magonjwa ya kiakili. Lakini mimi nimeona kinyume. Wagonjwa wengi huanzia kanisani na kwa waganga, na hivyo kabla yao kufika hospitali, hali yao huwa imekuwa mbaya sana.
"Je, waganga hawa wa asili wanaponya? Hilo ndilo swali kuu.”
Shirika la Mtakatifu Camille halina daktari yeyote wa magonjwa ya kiakili wa kudumu Benin, lakini hutembelea na madaktari kutoka Ulaya mara kwa mara.
Hufika na kukaa wiki kadha kila baada ya miezi kadha kupita.
No comments:
Post a Comment