Kaya 50 karibu na ghorofa 16 eneo la Indira Ghandi zapewa siku 3 kupisha zoezi la Kulibomoa - LEKULE

Breaking

3 Feb 2016

Kaya 50 karibu na ghorofa 16 eneo la Indira Ghandi zapewa siku 3 kupisha zoezi la Kulibomoa



Zaidi ya kaya 50 zinazoishi kuzunguka jengo la ghorofa 16 lililopo mtaa wa Indira Gadhi katikati ya jiji ambalo linatakiwa kubomolewa zimepewa siku tatu ziwe zimeondoka kwa muda ili kupisha zoezi hilo ambalo litachukuwa miezi mitatu hadi kukamilika.
 
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Saidi Mecky Sadiki ametoa agizo hilo mara baada ya kutembelea eneo hilo ambapo amesema lengo la wao kutakiwa kuondoka ni kunusuru maisha yao na kwamba baadhi ya barabara nazo zitafungwa huku akielezea sababu zilizochelewesha zoezi hilo la ubomoaji kuanza.

Baadhi ya wananchi wanaotakiwa kupisha zoezi hilo wamepongeza hatua hiyo na kudai kuwa walikuwa wanaishi kwa mashaka kwa kipindi chote hicho na wengine wakihoji utaratibu wa gharama za kuhama kwa madai kuwa hawana uwezo wa kwenda kupangisha hoteli miezi yote hiyo.

Akizungumzia zoezi hilo mkurugenzi wa manispaa ya Ilala Bw Isaya Mngulumi amesema baada ya kikao cha ulinzi na usalama cha mkoa kumalizika watatoa taarifa ya maandishi kwa wakazi hao ya kuhama

Uamuzi wa kubomoa jengo hilo umechukuwa zaidi ya miaka mitatu tangu lilipobainika kuwa limejengwa chini ya kiwango na halikuzingatia vibali vya ujenzi kwani lilipewa kibali cha kujenga ghorofa 10 badala yake wakajenga ghorofa 16.

No comments: