Kamanda Kova Ambwaga Tena Nzowa Mahakamani - LEKULE

Breaking

27 Feb 2016

Kamanda Kova Ambwaga Tena Nzowa Mahakamani


Mahakama ya Rufaa Tanzania, imetupilia mbali kesi ya kugombea nyumba namba 140 iliyopo eneo la Sekei Arusha baina ya makamishna wawili wa Jeshi la Polisi, Godfrey Nzowa, ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.

Aidha, mahakama hiyo imeamuru Nzowa kulipa gharama.

Akisoma jana maamuzi ya Mahakama yaliyotolewa na majaji watatu wa vikao vya mahakama ya rufaa vinavyoendelea Jijini Arusha, ambao ni Mwenyekiti wa jopo la kikao cha mahakama ya rufaa, Jaji Mbarouk Salum Mbarouk, Mussa Kipenga na Bernad Luanda, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Elizabeth Mkwizu, alisema kesi hiyo imeondolewa katika usikilizwaji wa vikao vya mahakama hiyo kwa sababu za kiufundi.

“Sababu ya kuondoa kesi hii ni mkata rufaa Nzowa… alichelewa kukata rufaa ndani ya siku 60 na hivyo kuwa nje ya sheria kama inavyotakiwa, ukitaka kukata rufaa, ukate rufaa ndani ya siku 60 tangu kesi ya msingi kutolewa hukumu,” alisema.

Mkwizu alisema mbali na kesi hiyo kuondolewa mahakamani, Mahakama ya Rufaa pia imeamuru Nzowa kulipa gharama za wajibu rufaa ambao ni Kova na Wakala wa Majengo (TBA).

Katika kesi hiyo, makamishna hao wanagombea nyumba ya serikali iliyopo maeneo ya Sekei ijini Arusha, ambapo Nzowa anapinga kuuziwa Kova nyumba hiyo ambayo wakati ikiuzwa kwa watumishi wa serikali yeye ndiye alikuwa akiishi humo.

Wakati huo Nzowa alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Arusha (RCO), wakati Kova alikuwa ameshahamishwa kikazi mkoani Arusha.

Nyumba hiyo ni moja ya zile walizouziwa watumishi wa serikali wakati wa serikali ya awamu ya tatu, chini ya Rais Benjamin Mkapa na kusimamiwa na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Rais John Magufuli.

Awali, akizungumza mahakamani hapo mbele ya majaji hao, wakili wa serikali, Sylvester Mwakitalu kwa niaba ya mjibu maombi wa pili, TBA, waliomba mahakama hiyo kutupilia mbali kesi hiyo kutokana na Nzowa kuchelewa kutoa kusudio la kukata rufaa.

Alisema upande huo wa waleta maombi, umekiuka utaratibu wa kisheria wa kukata rufaa ndani ya siku 60, ambapo wao walitoa kusudio la kukata rufaa Oktoba 3 mwaka 2014 na kwamba, Januari 2, 2015, ndipo rufaa yao iliwasilishwa kwa Msajili wa Mahakama.
 
Hoja hiyo iliungwa mkono na wakili Dilip Kesaria, anayemtetea Kamishana Suleiman Kova.

Hata hivyo, mawakili wa Nzowa, Neema Mtayangulwa na Mpaya Kamara, walipinga pingamizi hilo na kuomba mahakama hiyo iendelee usikilizwaji wa kesi kwani upande huo unachelewesha kesi pasipo sababu za msingi.

Alisema kuwa kimsingi, kusudio la kukata rufaa lilitolewa kabla ya kuanza uwasilishaji wa kesi na hivyo kesi hiyo inapaswa kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, Kamanda Kova alijaza fomu namba 27 Mei mwaka 2002 ya kuomba kununua nyumba hiyo iliyokuwa namba 203, kabla ya kubadilishwa kuwa namba 149, akidai ni makazi yake. Aliyekuwa akiishi katika nyumba hiyo kwa muda huo ni Nzowa.

Pamoja na kujaza fomu hizo, pia Kova alitoa fedha za kununua nyumba hiyo wakati Nzowa akiishi humo.

No comments: