IPTL Yakanusha Habari Zilizochapishwa na Gazeti La Jamvi La Habari Kwamba Wanalipwa Milioni 300 Kwa Siku na TANESCO - LEKULE

Breaking

4 Feb 2016

IPTL Yakanusha Habari Zilizochapishwa na Gazeti La Jamvi La Habari Kwamba Wanalipwa Milioni 300 Kwa Siku na TANESCO


  1. Makampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na Pan Africa Power Solutions (T) Limited (PAP), kwa masikitiko makubwa tumesoma taarifa mbali mbali zilizochapishwa na gazeti la kila wiki la Jamvi la Habari hususan toleo namba 90 la tarehe 1 Februari 2016 lenye kichwa cha habari, “Miezi 14 ya sakata la Escrow –Sethi na IPTL waikamua Tanesco milioni 300 kila siku”; iliyoambatana na dondoo saba zilizosomeka kama ifuatavyo:-
  • Ni malipo ya ‘Capacity Charges’
  • Ni mara mbili zaidi ya kashfa ya Richmond
  • Wanaharakati washangazwa na kimya cha serikali
  • Takukuru yatakiwa kuingilia kati
  • Waziri Muhongo aombwa kuchukua hatua madhubuti
  • Fedha wanazolipwa IPTL zinatosha kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge miaka 36
  • Yaelezwa ni sababu kuu ya gharama za umeme kupanda
  1. Tungependa kukanusha taarifa hizi. Kwanza kabisa, taarifa hizi ni uzushi mtupu wenye lengo la kuichafua IPTL na wamiliki wake akiwemo Mwenyekiti Mtendaji, Bwana Harbinder Singh Sethi. Pili, taarifa hizi ni za kichochezi kwani zinalenga kuwachonganisha wananchi wa Tanzania na serikali yao. Tatu, taarifa hizi zimechongwa na kuchorongwa ili kuwachonganisha wananchi wa Tanzania dhidi ya mwekezaji, IPTL/PAP na mwenyekiti wake mtendaji, Bwana Harbinder Singh Sethi; kwani inakusudia kuwahadaa Watanzania kuwa IPTL inanyonya rasilimali za nchi.
  1. Awali ya yote, tungependa kuutarifu umma wa Watanzania kwamba malipo ya tozo ya uwekezaji (“Capacity Charges”) yamo kwenye mikataba yote ya kufua na kuuziana umeme (Power Purchase Agreement –PPA) duniani kote, baina ya makampuni binafsi ya kufua nishati ya umeme (Independent Power Producers) na mashirika husika ya umma ya ugavi wa nishati ya umeme, kama ilivyo katika mkataba wa kuuziana umeme baina ya IPTL na TANESCO.
  1. Hata hivyo, si kweli kwamba IPTL inalipwa fedha za Kitanzania milioni 300 kwa siku kama “Capacity Charges” kama ilivyodaiwa na gazeti hilo la Jamvi la Habari. Kinacholipwa na TANESCO kwa IPTL kama “capacity charges” haijawahi kuzidi fedha za Kitanzania million 150 kwa siku tokea mradi wa kufua umeme wa IPTL ulipozinduliwa mwaka 2002 hadi leo.
  1. Tunashangaa kuona gazeti linalodai kuwa na waandishi weledi wakiandika taarifa ya upotoshaji zisizofanyiwa utafiti yakinifu kufahamu maana ya “Capacity Charges”; kwanini kampuni inalipwa hiyo “Capacity Charges”; namna gani hiyo “Capacity Charges” inavyokokotolewa; na kiasi gani halisi kinacholipwa kwa kampuni ya IPTL baada ya kuondoa kodi na gharama zingine mbalimbali husika.
  1. Gazeti la Jamvi la Habari pia inaeleza kwenye taarifa yake hiyo kwamba “Capacity Charges” inayolipwa IPTL ndiyo sababu kuu ya gharama za umeme kupanda. Huu ni uzushi mwengine. Jedwali la gharama za “Capacity Charges” zinazotozwa na makampuni mbali mbali binafsi zinazofua na kuiuzia umeme TANESCO (tunalolinukuu hapa chini), inadhihirisha wazi kuwa gharama za “Capacity Charges” inayolipwa kwa IPTL ziko chini ukilinganisha na gharama za “Capacity Charges” zinazolipwa kwa makampuni mengine binafsi zinazofua na kuiuzia umeme TANESCO.
Jedwali: Mlinganisho wa Gharama za Ununuzi na Kuuza kwa Uniti Moja (Kwh)
Tariff for EPPs and IPPs:
Rental Company
Energy Charge / kWh
Capacity Charge / kWh
Total Charge / kWh
Selling Price (USD / kWh)
Difference (USD / kWh)
Aggreko
0.369
0.0577
0.4267
0.1197
(0.307)
Symbion
0.284
0.0565
0.3405
0.1197
(0.2208)
Symbion (natural gas)
0.029
0.0499
0.0789
0.1197
0.0408
IPTL
0.13
0.0106
0.0106
0.1197
(0.1139)
Songas
0.0217
0.0431
0.0648
0.1197
0.0549
  1. Gazeti la Jamvi la Habari pia limehusisha malipo ya Capacity Charges yanayolipwa IPTL na gharama za kurusha matangazo ya moja kwa moja ya bunge katika runinga, likidai kwamba “Fedha wanazolipwa IPTL zinatosha kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge miaka 36”. Gharama za kufua umeme hazina uhusiano wowote na gharama za kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge. Kwa sababu malipo haya yanayolipwa kwa IPTL ni malipo yanayotokana na mkataba wa kufua umeme kati ya IPTL na TANESCO. Kuhusisha gharama hizi za “Capacity Charges” inayolipwa kwa IPTL kwa mujibu wa mkataba wa kufua umeme na gharama za kurusha ‘Live’ matangazo ya Bunge siyo tu ni uchochezi wa wananchi dhidi ya serikali yao bali pia ni uchochezi wa wananchi dhidi ya kampuni ya IPTL/PAP na mwenyekiti wake mtendaji Bwana Harbinder Singh Sethi, ambayo ni uvunjifu wa katiba na sheria husika za nchi.
  1. Mwandishi wa makala husika angeuliza IPTL ama TANESCO bila shaka angeweza kupata taarifa sahihi na ufafanuzi wa kutosha badala ya kukurupuka na kuandika mambo ya kizushi na uchochezi. Tungependa kutumia fursa hii kutoa rai kwa waandishi na vyombo vyote vya habari kuzingatia weledi wa fani zao katika kuandika taarifa sahihi ya mambo mbalimbali wanayoyaandika ikiwemo taarifa za kampuni ya IPTL, PAP na Bwana Harbinder Singh Sethi.
  1. Kwa muhtasari, taarifa zilichochapishwa kwenye makala husika ni uzushi usiokuwa na ukweli wowote. Tungewaomba Watanzania na wote waliosoma au watakaosoma makala husika wazipuuzie taarifa hizo. Pia tunawataka wahariri na wachapishaji wa gazeti la Jamvi la Habari kuomba radhi kwa taarifa hizo za kizushi ndani ya siku kumi na nne (14). Kushindwa kufanya hivyo, hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwemo kulifikisha gazeti pamoja na wahariri wake mahakamani.
  1. Tunaomba pia vyombo mbalimbali vinavyohusika na kulinda amani na utengamano wa nchi yetu ikiwemo jeshi la polisi kuwachukulia hatua mwandishi wa makala hiyo na wahariri wa gazeti la Jamvi la Habari kwa kuvunja sheria za nchi kwa kuandika habari za uchochezi.
Ahsanteni sana.
Joseph O. R. Makandege (ADVOCATE)
(Katibu na Mshauri Mkuu wa Sheria)
KAIMU MWENYEKITI MTENDAJI
Independent Power Tanzania Limited / Pan African Power Solutions (T) Limited.

No comments: