HUDUMA MPYA YA UPASUAJI KWA NJIA YA VITUNDU YAANZA KUTOLEWA RUFAA MBEYA - LEKULE

Breaking

18 Feb 2016

HUDUMA MPYA YA UPASUAJI KWA NJIA YA VITUNDU YAANZA KUTOLEWA RUFAA MBEYA

Wataalam wa Upasuaji wakiangalia namna ya kufanya upasuaji kwa njia ya vitundu



 Prof. Dr Med Henning Niebuhr.Kutoka Ujerumani akitoa maelekezo juu ya namna ya kufanya upasuaji kwa njia ya vitundu







Madaktari wakiwa kwenye Chumba cha upasuaji


Huduma mpya ya kitabibu imeanza kutolewa katika hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya itakayomuwezesha mgonjwa kufanyiwa upasuaji kwa njia ya vitundu (Laparoscopic surgery) na hivyo kumuwezesha mgonjwa kupona mapema na kuwahudumia wagonjwa wengi kwa muda mfupi. 
 Huduma hiyo ambayo inatumia mashine inayofahamika kwa jina la Mnara wa Upasuaji wa Vitundu au Laparascopic Tower inalenga kutumia muda mfupi wa upasuaji, na kumuwezesha kufanya mgonjwa kupata naafuu mapema. 
 
Akizungumza na mwandishi wetu daktari bingwa wa Upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Mbeya, Dkt. Lazaro Mboma amesema kuwa mashine hiyo itamuwezesha mgonjwa kurudi katika shughuli zake za kawaida muda mfupi baada ya upasuaji kutokana na kutokuwa na kidonda kikubwa badala yake mgonjwa atakuwa akiuguza vidonda vidogo vya matundu yaliyotumika wakati wa upasuaji tu. 
 Pamoja na hayo amesema kuwa kwa siku ya kwanza (leo) wagonjwa wawili waliokuwa na matatizo ya mawe katika mfuko wa nyongo wamefanyiwa upasuaji wa mafanikio ambapo kazi hiyo imekwenda sambamba na kuwapa mafunzo madaktari wengine wa hospitali hiyo juu ya matumizi ya mashine hiyo.  
Aidha Dkt. Lazaro Mboma alisema kuwa mashine ya Mnara wa Upasuaji wa Vitundu inawahusu wagonjwa wote, wale wanaotumia bima za afya na wasionazo lakini kutokana na gharama za uendesheji inawalazimu madaktari kuwahudumia kwanza wagonjwa wanaohudumiwa kwa bima ya afya kwani hivyo amewashauri wananchi kujiunga na mfuko wa bima ya afya kwani kwa mgonjwa wa kawaida ni ngumu kumudu gharama za matibabu. 
 Madaktari waliofika jijini Mbeya kwaajili ya kutoa mafunzo kwa madaktari wa hospitali hiyo ni daktari Prof. Hening na mtaalamu wa mashine hiyo Frolian Bets ambao wataendelea kuwepo jijini Mbeya kwa siku tatu ili kuwawezesha madaktari wa hospitali ya Rufaa Mbeya kupata ujuzi wa kutumia mashine hiyo. 
Naye mkuu wa idara ya upasuaji katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Mbeya Dkt. Mujuni Mutagwaba ametoa wito kwa wakazi wa Mbeya na mikoa ya nyanda za juu kusini kujitokeza kutibiwa katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya Mbeya ili kuokoa gharama na kupata tiba stahiki.  
Mashine ya kitabibu ya Mnara wa Upasuaji wa Vitundu (Laparoscopic Tower) ni ya kwanza mkoani Mbeya na ni vituo vichache Tanzania vilivyo na mashina ya upasuaji ya aina hii hivyo kupelekea wagonjwa wengine kusafiri kwenda nchi nyingine kwaajili ya kupata tiba kwa njia hii.

No comments: