DC Paul Makonda Aagiza Walimu wa Shule za Serikali Dar es salaam Wapande Daladala Bure - LEKULE

Breaking

28 Feb 2016

DC Paul Makonda Aagiza Walimu wa Shule za Serikali Dar es salaam Wapande Daladala Bure


Moja ya jambo ambalo serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa John Pombe Magufuli imelifanya kuwa kipaumbele kikubwa kwenye mipango yake ya kimaendeleo ni suala la uboreshaji wa sekta ya elimu nchini na ndio maana serikali imeanza utekelezaji wa mpango huu kwa kufuta ada zote mashuleni.

Kimsingi ni ndoto hii ya Mheshimiwa Raisi ambayo nina hakika kila mmoja wetu anaelewa ukubwa wa faida zake kwenye ujenzi wa Tanzania mpya na yenye wasomi na wataalamu wa kila namna tena wanaopatikana bila kuzingatia hali ya kipato cha familia anayotokea mwanafunzi, iliyonifanya mimi kama msaidizi wake katika nafasi ya ukuu wa wilaya nijiulize kila wakati juu ya ushiriki wangu wa kuhakikisha inatimia kikamilifu. 
Maswali ambayo yamenifikisha kwenye wazo la kuboresha sekta hii kwa kuchagua kufanya jambo ambalo wakati serikali ikiendelea kupigania changamoto nyinginezo za kuboresha ajira za walimu ikiwemo upandishwaji wa madaraja na mishahara, basi na mimi katika nafasi yangu nishiriki kwenye mchakato huu mzima kwa kutoa motisha ya usafiri wa bure kwa walimu wote wanaofundisha kwenye shule za serikali zilizopo jijini Dar es Salaam.

Kwa ufupi ni kwamba, wazo hili limejengwa juu ya msingi wa sababu kubwa tatu. Moja, kwa kuzingatia changamoto za nauli za mara kwa mara wanazolazimika kuzilipa walimu ili kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia kazi na pili, ni kuhakikisha mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni tunakuwa sehemu ya juhudi za Mheshimiwa Raisi za kuboresha maslahi na mazingira ya walimu ya kufanyia kazi ili matarajio ya ndoto yake anayoipigania usiku na mchana ya kutaka kuiona sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia. 
Na tatu, ni kuwafanya walimu wa wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla kama watumishi wenzangu wa serikali nao wanafaidi sehemu ya matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati imedhamiria kubadilisha maisha yao ili na wao waweze kubadilisha maisha ya vijana wetu kupitia taaluma.

Kwasababu hizo nilizozianisha hapo juu ninaomba kuwatangazia walimu wangu wa shule zote za serikali kuanzia za msingi mpaka sekondari ya kwamba, sasa watasafiri bure wanapokwenda kutufundishia wadogo zetu na watoto wao. 
Hii ni baada ya kufanya vikao na mazungumzo ya kina na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kupitia vyama vyao vya Darcoboa na Uwadar na hatimaye mazungumzo hayo kuitimishwa na mkutano wa vyama vyote hivyo viwili vya wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali kuniunga mkono kwenye utekelezaji wa wazo langu hili.

Kipekee na kwa unyenyekevu mkubwa, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wamiliki hawa wa vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi wa vyama vya Darcoboa na Uwadar kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa ukizingatia kuwa wao ni wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika sekta yao ya usafirishaji, wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili wapate uwezo wa kufanya biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao wameseme ndio na wako tayari kuanza haraka iwezekanavyo.

Utaratibu kwa walimu juu ya utumiaji wa fursa ambayo tumeipata utakuwa kama ifuatavyo:- Moja, nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi, kutoa maelekezo kwa wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu na wilaya nyinginezo za jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa na picha ya mwalimu, jina lake kamili, jina la shule anayofundisha, namba ya simu ya mkuu wa shule husika pamoja na saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda ili kuepuka udanganyifu.

Nimewataka zoezi hili walifanye na kulikamilisha ndani ya wiki moja ambapo baada tu ya kukamilika itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu wote wa shule za serikali jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda daladala bure ila tu kwa siku za jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda wa saa kumi na moja asubuhi mpaka saa mbili asubuhi na kati ya saa tisa mpaka saa kumi na mbili jioni. Ingawa, kila mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake alichotengenezewa kwenye shule yake pamoja na kile cha ajira ya serikali.

Imetolewa na:-
Paul Makonda

Mkuu wa wilaya – Kinondoni. 

No comments: