BARABARA MBOVU YAWATOA CHOZI WANANCHI WA MNYONZORI/KIBESA. - LEKULE

Breaking

4 Feb 2016

BARABARA MBOVU YAWATOA CHOZI WANANCHI WA MNYONZORI/KIBESA.

WAKAZI na wananchi wa vijiji vinavyounda Kata ya Panzuo, wilaya Mkuranga, mkoani Pwani, wameendelea kuililia barabara mbovu inayoanzia Kijiji cha Kimanzichana, hali inayowalazimu akina mama kujifungulia njiani na kuuweka uhai wao rehani.
Mwendesha bodaboda Ramadhan Rajab akijaribu kupita katika barabara mbovu inayotokea Kimanzichana, kuelekea vijiji vya Mnyonzole na Kibesa,wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, nauli kwa safari moja wakitoza Sh 20,000 hadi 30,000 kwa safari moja. Nyakati za mvua barabara hiyo haipitiki hali inayozidisha ugumu wa maisha kwa wananchi hao.



Vijiji hivyo ni Marui, Kisegese, Mbezi Muungwana, Msanga Visiga, Kibayani na vinginevyo vinavyoitumia barabara hiyo inayopitika wakati wa jua kali na zinapoanza mvua mawawasiliano yao kutoka katika maeneo yao hadi kwenye barabara Kuu ya Lindi Dar es Salaam kukosekana.


Mkazi wa kijiji cha Mnyonzole Kibesa, Cosmas Kisabo, akizungumza jambo kuhusiana na kero kubwa ya barabara wanayokutana nayo wananchi hao, inayaopelekea akina mama wengi kujifungulia njiani, mvua kubwa zinapoanza kunyesha.

Mwandishi wa mtandao huu ametembelea katika maeneo hayo na kujionea hali mbaya ya barabara hiyo ambayo inaweza kuwa chanzo cha kuinua uchumi wa wananchi hao endapo itakarabatiwa japo kwa kiwango cha changarawe ngumu.

Akizungumza jana wilayani hapa, dereva wa bodaboda anayejulikana kama Ramadhan Rajab, alisema kwamba mvua kubwa inaponyesha huwezi kutoka ulipokuwa kwenda sehemu yoyote, kwa sababu barabara inakuwa mbovu.
Mkazi wa kijiji cha Kibesa, Bi Sofia Michael anayejishughulisha na kilimo na biashara ndogo ndogo, akiwa nje ya kibanda chake akizungumza na mtandao huu. Bi Sofia anasema maisha yamekuwa magumu zaidi kutokana na kukosa barabara.

“Watu wa huku tunaishi magumu mno, maana hata sisi wa bodaboda hatuwezi kufanya kazi zetu vizuri ukizingatia kuwa watu wengi wanaoishi mjini wakija kwetu tunawasafirisha katika vijiji hivyo kwa shughuli zao mbalimbali kama vile biashara na kilimo, sasa anapokuta mvua hawezi kwenda popote, zaidi ya kuishia Kimanzichana na kurudi mjini,” alisema Rajab na kuiomba Halmashauri ya wilaya Mkuranga kuichonga barabara hiyo ili kuwafanya wananchi wajivunie kuishi katika maeneo hayo kwa ajili ya kuendelea na maisha yao.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kibesa, Khamis Ningwe akizungumza mtandao huu kutokana na kero kubwa wanazokutana nazo kila siku, ikiwamo barabara mbovu.
Barabara ya Mnyonzole inavyoonekana katika picha.
Barabara ya Mnyonzole inavyoonekana pichani, ikiwa ni siku chache baadaa ya kunyesha mvua kubwa na kusababisha adha kubwa kwa wakazi na wananchi wa maeneo hayo.

Naye mkazi wa kijiji cha Kibesa, aliyejitambulisha kwa jina la Sofia Michael, alisema ingawa kuna maeneo yenye kero kubwa, lakini kwao wamezidi, huku akisisitiza kukosekana kwa barabara hiyo ni sababu ya kuwafanya waishi porini bila msaada wowote na kukosa mahitaji muhimu kama vile chumvi,sukari, dawa na mengineyo.

“Mvua zinaponyesha huku kwetu tunaishi kama wanyama tu, maana hakuna mtu anayeweza kuleta bidhaa zake huku kwa sababu hana sehemu ya kupita, tunabakia kuishi kama watumwa au wafungwa na wakati mwingine mtu kupoteza maisha kwa sababu mbalimbali,yakiwamo magonjwa ambayo ili yapone yanahitaji tiba na tiba yenyewe inakuwa ngumu maana ili tufike hospitalini kunahitajika usafiri na njia yenyewe haipitiki,” alisema.

Mkazi mwingine aliyezungumza na mtandao huu ni Cosmas Kisabo, alisema hali ya maisha katika maeneo yao ni magumu kwa sababu hata wawekezaji wa aina yoyote wanashindwa kwenda kwao kwa kuhofia usafiri,jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kwa vitendo na viongozi na wadau kwa kushirikiana na wananchi wa vijiji vyao.

“Tunajua hali ni mbaya kwa watu wengi, lakini sisi huku tumezidi, maana hospitali zipo mbali na hauwezi kufika kwa wakati kutokana na kukosekana barabara, hivyo tunawaomba viongozi wetu watambue na sisi ni watu tunaohitaji maisha, watukarabatie barabara yetu hata kwa kiwango chochote tuone kama na sisi tutasonga mbele kiuchumi,” alisema Kisabo.

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Kibesa chenye kitongoji cha Mnyonzole, Khamis Ningwe, alisema kukosekana kwa barabara hiyo kunasababisha maisha yawe magumu, ndio maana hata viongozi wao wa chama na serikali huwatembelea kila mwaka wa Uchaguzi Mkuu kwa ajili ya kuwaahidi mambo mengi, ikiwamo barabara yao Kimanzichana hadi Mnyonzole.

“Tumeahidiwa sana,lakini hatuoni mwelekeo mzuri wa kutatuliwa kero zetu na maisha yanazidi kuwa magumu, maana mvua kubwa zinaponyesha, hayo mazao yako uliyovuna kama vile maembe,mananasi na bidhaa nyingine utaziangalia zinavyoshindana kuoza kwa sababu hakuna atakayekuja kuzinunua.

“Kiukweli hali hii tumeichoka kwakuwa inapelekea maisha yetu yanazidi kuwa magumu na changamoto zinakuwa kubwa zaidi, maana mimi kama mwenyekiti wakati mwingine nakutana na shida kubwa ya kusafirisha wagonjwa au wajawazito na kuanza kujiuliza maswali bila kupata jibu la uhakika, chanzo cha hayo ni barabara mbovu,” alisema.



Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga ina jimbo moja laUchaguzi, huku mbunge wake kwa sasa akiwa ni Abdallah Ulega, aliyepata nafasi hiyo katikauchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana.

No comments: