Ahadi Ya Rais Mtaafu Kikwete Yaibuliwa Bungeni - LEKULE

Breaking

3 Feb 2016

Ahadi Ya Rais Mtaafu Kikwete Yaibuliwa Bungeni



Ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Januari 25, mwaka 2008, jana ilizua maswali bungeni baada ya Mbunge wa Dimani (CCM), Hafidhi Ali Tahil, kuhoji ni lini Serikali itaanza kuitekeleza.

Mbunge huyo alisema kushindwa kutekelezwa kwa ahadi hiyo ya Rais mstaafu hadi sasa, inatafsiriwa na baadhi ya watu kuwa alilenga kuwadanganya wananchi.

Katika swali lake la msingi, Tahil alitaka kujua ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kichakapunda na ile ya kuunganisha umeme na maji kwenye Kijiji cha Jitimai hadi Skuli kama alivyoahidi Rais Kikwete kwenye moja ya ziara zake alizozifanya visiwani Zanzibar, 2008. 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Luhwaga Mpina, akijibu swali hilo, alisema ahadi hiyo imechukua muda mrefu, lakini iko mbioni kutekelezwa kama ilivyoahidiwa.

Mpina alisema Serikali itatekeleza ahadi zote zilizotolewa, na tayari ofisi ya Wilaya ya Magharibi viliko vituo hivyo, imeshafanya mawasiliano na wizara zinazoshughulikia sekta ya afya na umeme ili hatua za utekelezaji zianze.

“Kwa sasa wananchi wa Kichakapunda wanapata huduma za afya kupitia vituo vya afya vya Kibondeni, Melitano na Fuoni, ambavyo vyote umbali wake kutoka Kichakapunda hauzidi kilomita tatu,” alisema Mpina.

Alisema kwa mujibu wa Sera ya Afya ya Zanzibar, masafa hayo yanakidhi haja ya upatikanaji wa huduma hizo.

Alisema mipango ya kujenga kituo hicho cha afya bado inafanyiwa kazi wakati huduma ya umeme imekwishafika eneo la Hado.

No comments: