TAARIFA KWA UMMA.
Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. George Simbachawene (Mb) amemuagiza
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kumsimamisha kazi mara moja Kaimu Afisa
Biashara wa Manispaa ya Ilala Bw. Dennis. N. Mrema kuanzia leo tarehe
07 Januari, 2016 kwa kosa la kusababisha upotevu wa Mapato ya Serikali
kutokana na urasimu wa kukusudia, mazingira ya rushwa na uzembe katika
utoaji wa leseni za Biashara.
Kutokana
na hali hiyo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI ameelekeza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kumuondoa kwenye nafasi
yake Kaimu Afisa Biashara wa Manispaa ya Ilala na nafasi yake kukaimiwa
na mtu mwingine ili kupisha uchunguzi zaidi juu ya tuhuma zilizotolewa
dhidi yake.
Mhe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais –TAMISEMI amefikia uamuzi huu baada ya
kupokea malalamiko mengi kutoka kwa Wafanyabiashara ambao wamemlalamikia
Mtendaji huyu kwa ukiukwaji wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utoaji wa
Leseni za Biashara, Urasimu na Mazingira ya rushwa.
Katika uchunguzi wa awali uliofanyika kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Ilala mambo yafuatayo yamegundulika:
(i)Ukiukwaji wa Makusudi wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utoaji wa Leseni za Biashara.
(ii)Kutoa
Leseni za Biashara zaidi ya 843 bila kuwa na Vyeti vya uthibitisho wa
Walipa kodi ‘Tax Clearance Certificates” hivyo kukosesha Serikali Kodi
ya Mapato.
(iii)Kukaa na fomu za Wafanyabiashara 336 kwa muda mrefu bila sababu za msingi.
(iv)Kukiuka
Mwongozo wa Mkataba wa Huduma kwa wateja ambao unamtaka Afisa Biashara
kutoa Leseni za Biashara ndani ya siku 2 hadi 3 baada ya muombaji
kuwasilisha maombi yake ya kupatiwa Leseni ya Biashara.
Aidha,
Mheshimiwa Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais-TAMISEMI amewaagiza Maafisa
Biashara wote nchini watoe huduma za Leseni kwa kuzingatia Sheria,
Kanuni na Taratibu , kuacha urasimu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Ofisi ya Rais-TAMISEMI,
07 Januari, 2016.
No comments:
Post a Comment