Waziri Mkuu Afurahishwa na Hali ya Chakula Mkoani Ruvuma - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Monday, 4 January 2016

Waziri Mkuu Afurahishwa na Hali ya Chakula Mkoani Ruvuma

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU AFURAHISHWA NA HALI YA CHAKULA MKOANI RUVUMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefurahishwa na hali ya chakula mkoani Ruvuma, ikiwa kati ya mikoa inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi nchini.

Akizungumza na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali jana jioni (Jumapili, Januari 3, 2016) katika ukumbi uliopo Ikulu ndogo Songea, Waziri Mkuu  ameutaka  uongozi wa mkoa kuhakikisha kuna  upatikanaji wa masoko kwa mazao mbalimbali pamoja na kuendelea kutoa msukumo kwa wananchi.

Pia, ameupongeza uongozi wa mkoa huo kwa kutoa msukumo kwa wananchi na kufanyakazi, na kusema ni jambo linalosaidia kupanda kwa pato la mtu mmoja  mmoja, hata hivyo hakusita kuwashukuru kwa mapokezi makubwa aliyopata.

“Nawapongeza sana wana Ruvuma kwa kuongeza pato la ndani kutoka  shilingi 654,227, hadi kufikia shilingi 1,800,000 kwa kipindi cha mika 4 tuendelee kujiweka vizuri kwa kuongeza pato la mtu mmoja mmoja” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa pia amesisitiza  kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yote yenye mabonde ili wakulima waweze kuvuna bila kutegemea sana kipindi cha masika. Amesema ni lazima kuimarisha huduma muhimu na kusisitiza matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana  katika mazao hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu amesema  zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Ruvuma hutegemea kilimo cha mazao  mbalimbali ya chakula na biashara  yakiwemo mahindi, mpunga ambao unalimwa sehemu za Tunduru na Songea vijijini, korosho  ambazo zinalimwa sehemu za Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea vijijini na tumbaku  maeneo ya Namtumbo,Mbinga na Songea vijijini.

Alisema, Ruvuma imekua ikizalisha chakula kwa kiwango cha utoshelezi na ziada kwa kipindi cha mwaka 2012 - 2013, 2013 - 2014 hali hiyo imeendelea kuwa nzuri hadi kipindi cha mwaka 2015 - 2016. Mahitaji yakiwa ni tani 469,172 na ziada ikiwa tani 1,950,111, ametaja baadhi ya sababu za ongezeko hilo la tani  ni pamoja na matumizi ya dhana  bora za kilimo, matumizi ya pembejeo za kisasa na urahisi wa upatikanaji wa pembejeo, aliongeza Mkuu wa Mkoa.

Waziri Mkuu Majaliwa ambaye jana (Jumapili, Januari 3, 2016) ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Ruvuma, leo  siku ya jumatatu  atakuwa na shughuli za kufungua  tawi la Benki ya Posta mjini Songea, kukagua  maghala ya Wakala wa Taifa wa  Hifadhi ya chakula  (NFRA) kanda ya Songea na kukagua Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

Kupitia ziara hii Serikali ina lengo la kuona hali halisi ya utendaji wa shughuli za maendeleo kutoka kwa watendaji mbalimbali, kuwatia moyo na kuweka msisitizo  katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika sekta ya Afya.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P 3021,11410 -DAR ES SALAAM

JUMATATU, JANUARI 4, 2016.
Post a Comment