Baraza
Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata) pamoja na taasisi zake limeiomba
Serikali kutoa ufafanuzi masuala ya misamaha ya kodi kwa taasisi za dini
ili kuondoa changamoto zinazoweza kusababisha upendeleo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini hapa jana, mwenyekiti wa Taasisi ya
Kiislam ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis alisema kama utaratibu wa
kudai taarifa za matumizi ya misamaha ya nyuma umeanzishwa, Serikali
iwaweke wazi wanufaika wote wa misamaha hiyo na isiwaachie maofisa wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waifanye kazi hiyo.
Alisema
Novemba 19 mwaka jana, TRA iliandika barua kwa Baraza ikitaka ipatiwe
taarifa mbalimbali kwa lengo la kutoa msamaha wa gari moja aina ya Iveco
lililoombewa msamaha kama taasisi za dini zinavyofanya.
“Katika
barua ile, tuliambiwa tutoe taarifa hizo ndani ya siku saba na
tuambatanishe kazi za magari 82 yaliyoingizwa nchini tangu 2006, vitabu
vinavyoonyesha safari za magari hayo, majina ya madereva, risiti za
kulipia mafuta, bima, huduma za matengenezo na pia tuwasilishe ushahidi
wa fedha zinazotumika kununua magari hayo pamoja na hesabu za mwaka,” alisema Sheikh Khamisi.
Bakwata
ilisema katika kipindi cha miaka 10 kuanzia 2006 hadi 2015, baraza
pamoja na taasisi zake, ilipata misamaha ya kodi yenye thamani ya Sh1.9
bilioni.
Msamaha huo ni wa kutoa magari 82 bandarini yenye thamani ya Sh6.8 bilioni ikiwa ni wastani wa magari manane kwa mwaka.
Wakati
huo huo, ilielezwa kuwa misamaha ya kodi inayotolewa na TRA kwa taasisi
nyingine za dini zisizokuwa za Kiislamu katika kipindi hicho ilikuwa
Sh90 bilioni, sawa na magari 3,937 ya aina mbalimbali yaliyokuwa na
thamani ya Sh331 bilioni ambayo ni wastani wa magari 394 kwa mwaka.
“Takwimu
zinaonyesha kuwa Kanisa Katoliki pamoja na taasisi zake zimefaidika na
msamaha wa kodi ya jumla ya Sh19.5 bilioni kwa kuingiza magari 691 yenye
thamani ya Sh59 bilioni ambayo ni sawa na wastani wa magari 69 kwa
mwaka na msamaha huu ni takribani mara kumi na moja ya ule waliopewa
Bakwata,” alidai Sheikh Khamisi.
Alisema
katika kipindi hicho cha miaka 10, Jumuia ya Makanisa ya Kikristo
Tanzania (CCCT) pamoja na taasisi zake, ilipata msamaha wa kodi ya
Sh13.8 bilioni kutokana na kuingiza magari 527 yenye thamani ya Sh42.9
bilioni, sawa na wastani wa magari 53 kwa mwaka na kodi iliyosamehewa ni
zaidi ya mara 13 ya ile iliyosamehewa Bakwata na taasisi zake.
“Pia
Jumuiya ya Makanisa ya Kipentekoste Tanzania pamoja na taasisi zake,
walipata msamaha wa kodi wenye thamani ya Sh57 bilioni kutokana na
kuingiza magari 2,719 yaliyokuwa na thamani ya Sh186 bilioni ikiwa ni
wastani wa magari 272 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na
msamaha huu ni zaidi ya mara 30 ya msamaha waliopatiwa Bakwata,” alifafanua.
Alisema
mbali na msamaha wa taasisi hizo za dini, pia jumuiya za Wahindu na
Mabudha pamoja na taasisi zao walipatiwa msamaha wa kodi wa Sh9 bilioni
baada ya kuingiza magari 203 yaliyokuwa na thamani ya Sh36 bilioni
ambayo ni sawa na wastani wa magari 20 kwa mwaka na msamaha huo ni mara
tano ya waliopatiwa Bakwata.
Alisema
kutokana na misamaha hiyo, Baraza kwa niaba ya Waislam, wametilia shaka
msimamo wa TRA wa kuwataka wapeleke vielelezo vya magari 82
yaliyosamehewa kodi katika kipindi hicho cha miaka 10.
“Baada ya kufanya mashauriano na taasisi nyingine, tunachukua nafasi hii kuiomba Serikali itupatie ufafanuzi,” alisema.
No comments:
Post a Comment