Waziri Kitwanga Atangaza vita ya Bodaboda - LEKULE

Breaking

18 Jan 2016

Waziri Kitwanga Atangaza vita ya Bodaboda


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga amesema katika kuhakikisha Serikali inapambana na uhalifu, Jeshi la Polisi limeanza ukaguzi maalumu wa bodaboda na kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu ili kufuatilia matukio mbalimbali.

“Kutokana na majambazi kubuni mbinu mpya kila siku, ikiwamo ya kutumia bodaboda kuvamia benki na wanaotoka benki na kuwapora fedha, kuanzia sasa bodaboda, hasa aina ya boxer zitasimamishwa wakati wowote na kupekuliwa,” alisema Kitwanga

Alisema polisi wameweka ulinzi maalumu na waendesha bodaboda watakaooneka kupakia kitu chochote na kukiweka mbele (katika tenki la mafuta) au kiti cha nyuma, watasimamishwa na kupekuliwa kwa maelezo kuwa maeneo hayo ndiyo hutumika kuficha silaha.

“Tunaomba wananchi watuvumilie kipindi hiki tukipambana na bodaboda kutokomeza uhalifu,” alisema.

Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya wananchi kuvamiwa na kuporwa fedha, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuzichukua benki huku wafanyakazi wa benki wakidaiwa kuhusika kutoa taarifa za wateja.

Mara zote majambazi hutumia bodaboda kufanikisha uhalifu huo, huku wakiwa na silaha ambazo huzitumia kutishia, kujeruhi na wakati mwingine kuua.

Tukio la hivi karibuni ni la Desemba 28 mwaka jana, ambako majambazi waliokuwa katika bodaboda walimvamia meneja wa operesheni wa kampuni ya simu za mkononi ya Zantel, Gabriel Raphael na kumpora Sh10 milioni na kumuua kwa risasi.

Kuhusu ujambazi huo, Kitwanga alisema watu wanaovamiwa na kuporwa fedha, wengi hutokea katika benki za ndani si za nje.“... Hii inatokana na utaratibu wa malipo katika benki hizi. Kwa mfano, benki za nje ukiwa na hundi inapitiwa na watu wachache tofauti na benki za ndani ambazo hupitiwa na watu wengi.”

“Inawezekana katika mlolongo huo wa benki za ndani kukawa na wafanyakazi wanaoshirikiana na majambazi. Tunachokifanya sasa ni kuongeza ulinzi tu wa askari.”

Kuhusu CCTV, Kitwanga ambaye pia ni mbunge wa Misungwi alisema teknolojia hiyo itasaidia kubaini matukio ya uhalifu na kwamba tayari Serikali imeshazungumza na China kuhusu upatikanaji wa kamera hizo, “Ufungaji wa utaanza mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai na tutaanzia Dar es Salaam.”

Alisema Jeshi la Polisi lina askari wachache ambao hawawezi kuwapo kila eneo, hivyo mpango wa kuweka kamera hizo ni kuhakikisha kila jambo linafuatiliwa kwa ukaribu.

“Wapo waliokamatwa wakituhumiwa kuhusika katika matukio ya kuwapiga watu risasi na kuwapora fedha. Baadhi yao wamekiri kuhusika na wengine wamekana,” alisema Kitwanga.


Alipoulizwa silaha zinazotumika zinatoka wapi, alisema, “wanazopewa raia kihalali hazitumiki katika matukio haya. Ni zile zinazoingia nchini kinyemela.”

No comments: