Watumishi wa Umma mnakumbushwa tena kuvaa beji zenye majina yenu. - LEKULE

Breaking

26 Jan 2016

Watumishi wa Umma mnakumbushwa tena kuvaa beji zenye majina yenu.




Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ameagiza na kusisitiza ofisi zote Umma kusimamia na kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kila watumishi awe na kitambulisho (beji) kinachoonesha jina lake.

Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Balozi Sefue alisema hatua hiyo ya watumishi wa umma kuvaa beji zenye majina kila wakati wanapotekeleza majukumu yao itasaidia wananchi kuwatambua kwa majina watumishi wanaowahudumia na kuwasaidia kulingana na mahitaji yao kwenye ofisi hizo.

Ili kutekeleza azma ya kuwahudumia wananchi, Balozi Sefue alisema kuwa kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae beji zenye majina yao iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.

Zaidi ya hayo, Balozi Sefue amewahimiza viongozi na watumishi wote katika Utumishi wa Umma kubadilika kwa dhati kwenye utendaji na uadilifu wao na kuwahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima.

“Rais na sisi wote tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine, tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua” alisema Sefue.

Mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na kila kiongozi na mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi ili kuchukua hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.

Balozi Sefue amewahimza viongozi na watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima ambapo kila ofisi ya Serikali inapaswa kuwa na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

Kwa upande wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wote nchini wametakiwa kujenga uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati.

“Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu ndiye anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu, ikibidi wananchi wafike Ikulu inamaana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao” aliongeza Balozi Sefue.

Aidha, Balozi Sefue alisema kuwa ofisi zote za Serikali zinatakiwa kuwa na dawati la kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma inayotolewa.

No comments: