Mbunge wa CHADEMA Atimuliwa Kwenye kikao na Polisi - LEKULE

Breaking

26 Jan 2016

Mbunge wa CHADEMA Atimuliwa Kwenye kikao na Polisi



Mbunge wa Kilombero, Peter Elijualikali jana alijikuta akitolewa nje ya kikao cha Halmashauri ya Kilombero na jeshi la polisi kwa amri ya Mwenyekiti wa kikao hicho kwa madai kuwa sio mjumbe halali wa kikao hicho, hivyo haruhusiwi kupiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.

Sintofahamu hiyo iliibuka wakati Halmashauri hiyo ikijipanga kufanya uchaguzi wa Mwenyekiti wake, ambapo Mwenyekiti wa kikao alimtaka mbunge huyo kutoka nje kwa madai kuwa sio mjumbe halali na alipogomea agizo la mwenyekiti, aliondolewa nje kwa nguvu na polisi.

Mwenyekiti wa kikao hicho alieleza kuwa wamepokea ufafanuzi kutoka TAMISEMI kuwa mbunge huyo wa Kilombero anapaswa kuwa mjumbe wa vikao vya Halmashauri mpya ya Ifakara na sio halmashauri ya Kilombero.

Hata hivyo, maelekezo hayo yalipingwa vikali na madiwani wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa pamoja na mbunge huyo ambaye alieleza kuwa amepanga kwenda mahakamani kudai haki yake.

“Waziri wa TAMISEMI kama hataki kuchafuka na Katibu Mkuu wake, naomba wafanye kila wanaloliweza nirudi kwenye Halmashauri yangu. Na wasipofanya hivyo, nakwenda Mahakamani,” alisema Elijualikali.

Hatua hiyo ya kumtoa mbunge huyo na kumuelekeza kuhudhuria vikao vya halmashauri ya mji wa Ifakara ilitafsiriwa na madiwani wa Ukawa kuwa ni mbinu ya kutaka kupunguza idadi ya wajumbe wa vyama hivyo ili kuwezesha CCM kushinda nafasi ya Umeya wa Halmashauri hiyo.

Idadi ya wajumbe halali wa Ukawa ni 19 huku wa CCM wakiwa 18. Hata hivyo, Halmashauri ya Ifakala haina Mbunge kwakuwa sio jimbo. Hivyo, hiyo ni sababu ya kumuelekeza Mbunge huyo kuwa sehemu ya Halmashauri hiyo.

No comments: