Baada
ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, kuipiga chini kesi
iliyokuwa ikimkabili mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Esther Bulaya,
wadai katika kesi hiyo wanatarajiwa kupinga uamuzi huo Mahakama ya
Rufani.
Mwanasheria wa wadai hao, Constantine Mutalemwa, jana alisema wateja wake hawajaridhika na hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Gwae.
Juzi
katika mahakama hiyo, Bulaya aliwashinda wakazi wanne wa jimbo hilo
waliofungua kesi ya kumpinga baada ya ushindi alioupata kwenye uchaguzi
mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana. Katika uchaguzi huo, Bulaya olimshinda
mpinzani wake, Stephen Wasira wa CCM.
Bulaya, katika kesi hiyo, alikuwa akitetewa na mwanasheria maarufu, Tundu Lissu.
Waliofungua
kesi hiyo ni Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Ascetic
Malagira, ambao walikuwa na mawakili wawili ambao ni Mutalemwa na Denis
Kahangwa.
Mutalemwa
alisema baada ya kutoridhika na uamuzi huo, wateja wake wamekusudia
kufungua kesi Mahakama ya Rufani ili kupata ufafanuzi wa Jaji juu ya
uhalali wao wa kutokuwa na mamlaka kisheria ya kufungua kesi kama hiyo.
Katika
hatua nyingine, kesi ya madai iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda
ya Mwanza na mbunge wa zamani wa Nyamagana (Chadema), Hezekiah Wenje,
jana iliahirishwa hadi Februari 2, mwaka huu.
Uamuzi
wa kuahirisha kesi hiyo, ulitolewa na Jaji Joaquine De Mello wa
mahakama hiyo, aliposikiliza kwa muda kabla ya kupangiwa jaji wa
kuisikiliza kesi hiyo ya kupinga ushindi wa Stanslaus Mabula (CCM).
No comments:
Post a Comment