Mkurugenzi
wa Mikopo na Biashara wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),
Bw. Robert Pascal (Kulia) akimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Huduma za
Kisheria wa Benki, Bibi Neema Christina John (aliyevaa miwani) wakati wa
uhakiki wa fomu zilizojazwa na moja kati ya vikundi vilivyofanikiwa
kupata mkopo kutoka Benki hiyo.
Mwanasheria
mwandamizi wa TADB, Bibi Salome Masenga (Kulia) akimuelekeza mmoja wa
wanakikundi waliopata mikopo kutoka Benki hiyo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),
Bibi Rosebud Kurwijila (Aliyesimama) akiwapungia wakulima waliojitokeza
wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na
wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa,
wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Wajumbe
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),
wakiwapungia wakulima waliojitokeza wakati wa hafla ya utiaji saini
makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa
Iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB),
Bibi Rosebud Kurwijila (Kushoto) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bibi
Amina Masenza (Kulia) wakifuatilia kwa makini matukio wakati wa hafla ya
utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na wakulima wadogo
wadogo wa mkoa wa Iringa, katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi
mkoani Iringa.
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas
Samkyi (Kushoto) akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bw. Kasunga
(Kulia).
Mkurugenzi
Mwendeshaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw. Thomas
Samkyi (aliyesimama) akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Na Mwandishi wetu, Iringa
Wakulima
wote nchini wameaswa kutumia vizuri mikopo wanayopewa ili kuweza
kutimiza malengo yao binafsi na ya Serikali katika kusaidia upatikanaji
wa utoshelezi na usalama wa chakula ambao ni endelevu nchini Tanzania.
Wito
huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mama Amina Masenza wakati wa
wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya TADB na
wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa iringa, katika kijiji cha Igomaa,
wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Mama
Masenza alisema kuwa wakulima wakitumia mikopo waliyopewa kwa malengo
husika watafika mbali na kuweza kuchagiza mikakati ya Benki hiyo katika
kusaidia Mapinduzi ya Kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha
kilimo kibiashara ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini.
“Naamini,
wakati Benki ya Maendeleo ya Kilimo itapoanza kufanya tathmini ya
mikopo hii iweze kuona matunda ya uwekezaji wake hasa kwa nyie ambao
mmeweza kubahatika kupata fursa ya awali kabili kunufaika na huduma za
TADB,” aliwasihi.
Mama
Masenza aliwaomba wakulima hao kuwa Mfano Bora na wanaojitambua
vilivyo, hasa nia ya kutoka katika kiwango fulani cha maisha kwenda
katika hatua nyingine za juu zaidi kimaisha kwa kuongeza kipato na ubora
wa kimaisha kwa ujumla kupitia huduma za TADB.
“Nawasihi
kutotumia pesa hizi kinyume na malengo yaliyokusudiwa, kwani kwa
kufanya hivyo, siyo tuu tunaiua Benki yetu bali pia tunajimaliza wenyewe
kiuchumi. Wito wangu kwenu ni kujipanga kwa dhati ili kuweza kutimiza
malengo makuu ya mikopo hii ambayo ni kuleta Mapinduzi yenye tija katika
Sekta ya Kilimo nchini kwa kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri
zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini,” aliongeza.
Naye,
Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Bw. Thomas Samkyi amesema kwamba Benki
yake imedhamiria kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo
nchini ili kuchagiza na kusaidia kuwezesha Sekta ya Kilimo kutoka kilimo
cha kujikimu kwenda kilimo cha kibiashara ili kukuza uchumi na
kupunguza umaskini nchini.
Bw.
Samkyi alisema TABD imejizatiti kuchangia kwa kiasi kikubwa katika
mapinduzi ya kilimo kwa kuongeza tija na upatikanaji wa mikopo ya riba
nafuu maalum kwa sekta ya kilimo, kama njia ya kuleta Mapinduzi yenye
tija kwa wakulima nchini.
“Benki
imejipanga kutoa mikopo yenye riba nafuu katika muda mfupi, wa kati na
mrefu kwa Wakulima wadogo wadogo, wa kati na wakubwa, hususan kuziba
pengo la upatikanaji wa fedha za kwenye mnyororo wa ongezeko la thamani
katika tasnia za kilimo, mifugo, uvuvi na mazao ya misitu (ufugaji
nyuki),” alisema Bw. Samkyi.
Mkurugenzi
huyo alisema kwamba kwa kuanzia walengwa wakuu wa TADB ni wakulima
wadogo wadogo, hatahivyo, hata wale wakulima wa kati na wakubwa
watahudumiwa.
Bw.
Samkyi imejidhatiti katika kufanya tathmini ya kina katika mnyororo
mzima wa thamani ili kutambua mapengo na mapungufu yanayohitaji utatuzi
kwa minajili ya kuongeza thamani na ushindani kwenye masoko.
“Sera
ya TADB ni kutathmini mnyororo mzima wa thamani ili kutambua mapengo na
mapungufu yanayohitaji utatuzi, na ambayo utatuzi wake utaongeza tija na
uwezo wa ushindani kwenye masoko, na hivyo kukuza uchumi wa walio wengi
na kupunguza umaskini,” aliongeza.
Katika
hafla hiyo, jumla ya vikundi nane (8) vyenye jumla ya wakulima wadogo
wadogo 857, vilimiza vigezo na kupewa mikopo yenye thamani ya zaidi ya
shilingi bilioni moja.
Kwa
mujibu wa Bw. Samkyi kabla ya kutoa mikopo hiyo, benki iliwatembelea na
kutoa elimu kwa wakulima jinsi ya kuimarisha vikundi vyao, ambapo jumla
ya vikundi 89 vyenye jumla ya wanakikundi 21,526 vilifikiwa.
Akizungumzia
malengo ya TADB kwa upana, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki
hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila alisema kuwa Benki inalenga kutelekeza kwa
vitendo Maelekezo ya Serikali ya kupunguza changamoto zinazomkabili
mkulima.
“Tunalenga
kuwafikia wakulima wote nchini kadri siku zinavyoendelea kwenda na
kutegemea mtaji unavyoongezeka ama upatikanaji wa fedha toka vyanzo
mbali mbali ili kuweza kuwawezesha kumudu shughuli zao za kilimo,”
alisema.
Aliongeza
kuwa kwa sasa Benki inalenga kusambaa nchi nzima kwa kuanzisha Ofisi za
Kikanda ndani ya miaka mitano ijayo, kuwajengea uwezo na kuanzisha
Programu Maalumu ya Vijana wajihusishao na shughuli za Kilimo cha
kibiashara na kushirikiana na wadau wengine kuhuisha shughuli za
umwagiliaji na miradi ya kisasa ya umwagiliaji.
Malengo
mengine ni kutafuta fedha toka vyanzo mbalimbali zenye gharama nafuu
kwa minajili ya kuwakopesha Wakulima katika hatua zote za mnyororo wa
ongezeko la thamani kwenye mazao ya Kilimo na kupanua wigo wa utaoji
mikopo toka Minyororo Kumi na Minne (14) ya Mwanzo na kuhusisha pia
mazao mengine ya Kilimo na pia kuwaunganisha Wakulima na masoko ya ndani
na nje ya nchi.
Benki
ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilizinduliwa Rasmi na Rais wa Awamu ya
Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,
kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wakulima nchini, mnamo tarehe 8
Agosti 2015 mjini Lindi. Uanzishwaji wa Benki hii ni utekelezaji wa
malengo ya muda mrefu ya Serikali, katika kuitikia wito wa wananchi na
wadau wengine wa maendeleo ili Tanzania iweze kupiga hatua endelevu za
kimaendeleo.
No comments:
Post a Comment