Wageni Wote Wanaoishi Nchini Na Kufanya Kazi Kinyume Cha Sheria Kukamatwa - Masauni - LEKULE

Breaking

7 Jan 2016

Wageni Wote Wanaoishi Nchini Na Kufanya Kazi Kinyume Cha Sheria Kukamatwa - Masauni


Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeiagiza Idara ya Uhamiaji nchini kuanza Operesheni maalum ya kuwabaini wageni walioingia na kufanya kazi ambazo sio za kitaalamu zinazoweza kufanywa na Watanzania ili kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwaondosha.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhandisi Hamad Masauni baada ya kutembelea Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini jijini Dar Es Salaam na kuzungumza na makamishna wa idara hiyo.

Akiwa katika ofisi hizo kukagua shughuli zinazoendelea kwenye idara hiyo, Naibu waziri huyo amesema, kumekuwa na ongezeko kubwa la wageni wasikuwa na tija katika nchi ambao wengi wao wamekuja na kuomba vibali vya uwekezaji au kazi za kitaalam badala yake wamekuwa wakifanya kazi na biashara ambazo Watanzania wa kawaida wanaweza kuzifanya.


Naibu Waziri Masauni ameitaka idara hiyo kungalia Upya mchakato wa utoaji wa vibali kwa wageni baada ya vile vya awali kuonekana kuwa na matatizo.
Afisa Uhamiaji mkoa wa Dar es Salaam, Naibu Kamishna, Johannes Msumule akizungumza katika mkutano na Waandishi wa Habari ambapo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Hamad Yussuf Masauni alizungumzia hatua zinazochukuliwa na Wizara kudhibiti wageni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume na sheria. Mkutano huo ulifanyika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, jijini Dar es Salaam
 Sehemu ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Hamad Yussuf Masauni, wakati wa mkutano wa kuzungumzia hatua zinazochukuliwa na Wizara kudhibiti wageni wanaoishi nchini na kufanya kazi kinyume na sheria. Mkutano huo ulifanyika Makao Makuu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi jijini Dar es Salaam.

(Picha Na Kitengo Cha Mawasiliano Ya Serikali – Wizara Ya Mambo Ya Ndani Ya Nchi).

No comments: