TAARIFA KWA UMMA
Kumekuwa
na upotoshwaji kuhusu zoezi la ufuatiliaji wa matumizi ya misamaha ya
kodi inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa
wafanyabiashara, wawekezaji, Taasisi za Dini na Taasisi zisizo za
kiserikali kwa maelezo kwamba TRA inazilenga baadhi ya Taasisi.
Sheria
ya Mamlaka ya Mapato Tanzania inaipa Mamlaka ya kusimamia, kukagua na
kuhakiki mapato ya Serikali pamoja na kuzuia ukwepaji wa kodi wa aina
yoyote ile ikiwemo matumizi mabaya ya misamaha ya kodi inayotolewa kwa
mujibu wa Sheria.
Kifungu
cha 5 (3) cha Sheria ya TRA kinatoa mamlaka kwa TRA kufanya jambo
lolote lenye tija na manufaa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu
yake kisheria.
Kwa
vile misamaha ya kodi inatolewa kwa mujibu wa Sheria zinazosimamiwa na
TRA, ni wajibu wa Mamlaka kuhakiki kama bidhaa au huduma zilizosamehewa
zinatumiwa na watu au Taasisi zinazostahiki misamaha hiyo au kwa miradi
iliyokusudiwa.
Hivi
karibuni kumekuwepo na taarifa za upotoshaji kwamba TRA imeilenga
Taasisi moja ya kidini kwa kuiandikia barua ya kuomba vielelezo na ufafanuzi juu ya misamaha ya magari iliyopewa awali na kuonekana kana kwamba ni utaratibu mpya wa utoaji wa misamaha.
Tungependa kufafanua kwamba TRA haibagui wala kulenga Taasisi yoyote bali inatekeleza wajibu wake wa kufuatilia misamaha iliyotolewa
Katika
kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2015 TRA iliwaandikia walipakodi
65 kupata vielelezo juu ya matumizi ya misamaha ya kodi walioipata na
katika hao zimo Taasisi za kidini 39.
Ukaguzi
huu huisadia TRA kupata taarifa muhimu ili kuishauri Serikali namna
bora ya kutoa misamaha kwa ajili ya kuleta tija na ufanisi uliokusudiwa
ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii na kupunguza
umaskini.
Aidha
taarifa za misamaha ya kodi zinaisadia TRA kubaini matumizi bora ya
misamaha pamoja na mianya ya upotevu wa mapato kupitia misamaha hiyo ili
TRA ichukue hatua zinazostahili pale inapobainika kuwa kuna ukwepaji na
kuziba mianya hiyo.
Zoezi
hili ni endelevu hivyo tunaziomba Taasisi zote za kidini na mashirika
yote yanayonufaika na misamaha ya kodi kuchukulia zoezi la ukaguzi wa
misamaha hiyo kuwa ni utekelezaji wa sheria na wahusika wote watoe
ushirikiano kwa TRA pale wanapohitajika ili zoezi hilo lifanyike kwa
ufasaha na kwa manufaa kwa wote.
"Pamoja Tunajenga Taifa Letu"
A. J. Kidata
KAIMU KAMISHNA MKUU
No comments:
Post a Comment