Baadhi
ya Miwa iliyoteketea kwa moto kutokana na hujuma iliyofanywa na Watu
wasiojuilikana huko kwenye mashamba ya Miwa ya Kiwanda cha Sukari
Mahonda Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimpa Pole Meneja wa
Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana Tushar Mehta kufuatia watu
wasiojuilikana kutia tena moto mashamba ya Miwa Mahonda.
Balozi
Seif kati kati akifuatana na Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda
akikagua baadhi ya sehemu ya shamba la Miwa la Eka 50 lililotiwa moto
jana jioni na watu wasiojuilikana.
Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa.
Meneja
wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana Tushar Mehta akimueleza
Balozi Seif hasara iliyopatikana kutokana na hujuma ya moto kwenye
mashamba ya Miwa Mahonda.
Balozi
Seif akielezea masikitiko yake kutokana na baadhi ya watu kufanya
hujuma za makusudi kujaribu kuvuruga juhudi za Uongozi wa Kiwanda cha
Sukari Mahonda za kuimarisha Sekta ya Viwanda.
TISHIO la ajira za Wafanyakazi 350 wa Kiwanda cha Sukari Mahonda
zinaendelea kuwa hatarini kufuatia hujuma zinazofanywa kwa makusudi na
baadhi ya watu kuendelea kutia moto mashamba ya miwa huko Mahonda Mkoa
wa Kaskazini Unguja.
Kitendo hicho cha hujuma kinaweza kuusababisha Uongozi wa Kiwanda
cha Sukari Mahonda kuwa na mawazo ya kufikiria kuzuia ajira mpya 450 za
Wafanyakazi wa Kiwanda hicho katika malengo yake baada ya kukamilika kwa
matengenezo makubwa na kuanza tena uzalishaji wa sukari.
Meneja wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana Tushar Mehta
alisema hayo wakati akimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi aliyefika kuangalia hasara iliyosababishwa na moto
uliotiwa kwa mara nyengine tena na Watu wasiojuilikana ndani ya shamba
la Miwa katika kipindi cha siku Tano baada ya tukio kama hilo la Tarehe
30 mwezi uliopita.
Bwana Tushar alisema moto huo umetiwa kati kati ya shamba la Miwa
jana jioni na wahalifu wenye dhamira ya makusudi ya kutoa usumbufu na
kizuizi kwa wananchi na vikosi vya Ulinzi katika harakati za kukabiliana
na moto huo. .
Alisema Eka zipatazo 50 za Miwa iliyopevuka imeteketea kwa moto
hali ambayo imeisababishia Kiwanda hicho hasara ya Tani 200 za Sukari na
Lita 2,300 za Spititi zilizokuwa zizalishwe kutokana na miwa hiyo ikiwa
na hasara ya jumla ya dola za Kimarekani Laki 228,758.56 sawa na zaidi
ya shilingi Milioni 494 za Kitanzania.
Meneja huyo wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda alifahamisha
kwamba hadi sasa Eka zipatazo 200 zimeteketea kwa moto kwenye matukio
yote mawili katika kipindi cha siku Tano zilizopita na kusababisha
hasara ya jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 1,176,234.28 sawa na
shilingi za Kitanzania Bilioni 2,326,818,500/-.
Akiupa pole Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda kutokana na
hasara ya Mashamba iliyosababishwa na moto huo Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema hujuma hiyo ya makusudi haiitakii
neema Zanzibar katika harakati zake za kustawisha uchumi wake.
Balozi Seif aliwanasihi watu wenye tabia hiyo kuachana nayo kwani
mbali ya kujibebesha dhambi lakini pia inawavunja moyo wawekezaji
walioamua kuja kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Nchini kwa lengo la
kuisaidia Serikali pamoja na Wananachi hapa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba juhudi za
makusudi za Serikali kuu katika kukifufua tena Kiwanda cha Sukari na
Manukato Mahonda baada ya kusita kwa miaka kadhaa zililenga
kuimarisha Uchumi kupitia sekta ya viwanda sambamba na kupanua soko la
ajira kwa Vijana.
Alisema tabia ya baadhi ya watu kufikiria kwamba hujuma hiyo
itatoa fursa kwao kutumia maeneo ya mashamba ya Miwa kuendeleza Kilimo
na Mifugo inafaa kuachwa mara moja kwa vile mashamba hayo yataendelea
kuwa katika mipango ya Serikali ya kuhudumia Sekta ya Viwanda.
“ Haya ni Mashamba ya Serikali yaliyotengwa maalum kwa shughuli za
harakati za Viwanda. Hivyo ndoto za baadhi ya Watu kufikiria kwamba
hujuma zao zitazaa matunda kwa kufanya wanavyotaka zinapaswa ziachwe
mara moja ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliufahaisha Uongozi wa Kiwanda
cha Sukari Mahonda kwamba Serikali Kuu inaangalia mpango utakaowezesha
Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusaidia ulinzi kwenye
Mashamba hayo ili kulinda hujuma zinazoonekana kushamiri siku hadi siku.
Hilo ni tukio la sita la hujuma za moto kwenye mashamba ya Miwa ya
Kiwanda cha Sukari Mahonda tokea kianze tena uzalishaji wa sukari na
Spiriti mapema mwaka uliopita wa 2015.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
4/1/2016.
No comments:
Post a Comment