KAMPUNI
ya Simu Tanzania TTCL na Benki ya TIB leo zimetiliana saini Mkataba wa
makubaliano ya dhamana ya Benki na Mkopo wa Dola za Marekani Milioni 22
ikiwa ni awamu ya kwanza ya mkopo wa Dola za Marekani milioni 329
itakazopewa TTCL.
Akizungumza katika hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya mkopo
huo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Dk. Kamugisha Kazaura alisema mkopo
huo ni mahususi kwa ajili ya kuiwezesha TTCL kusimika mitambo mipya na
ya kisasa kuboresha huduma zake kwa kujenga na kusambaza huduma za
Mitandao ya 3G na 4G LTE nchini kote.
Dk. Kazaura alisema hatua hiyo ni habari njema kwa Watanzania,
hasa wateja na wadau wa huduma za kampuni ya TTCL. “…TTCL inaishukuru
sana Benki ya TIB kwa kutuamini na kukubali kushirikiana nasi baada ya
kujiridhisha kuwa tunao uwezo na nia thabiti ya kufanya mageuzi makubwa
ya kibiashara ili kuboresha huduma zetu,” alisema Dk. Kazaura
akizungumza.
“Kupatikana kwa mkopo na dhamana hizi kutapunguza tatizo la
ukosefu wa fedha lililokuwa linatukabili na sasa tutaweza kutekeleza kwa
kasi mpango wetu wa mageuzi ya Ki biashara ikiwa ni pamoja na kujenga
miundombinu, kuleta mitambo na vifaa vya kisasa vitakavyoongeza ufanisi
katika huduma zinazotolewa na TTCL kwa Wateja wa ndani na nje ya nchi.
Natoa wito kwa Watanzania na Wateja wetu wote kwa ujumla waendelee
kutegemea huduma na bidhaa zenye viwango vya juu kabisa vya ubora,
uhakika na gharama nafuu kutoka TTCL.” Amesema Dk. Kazaura.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIB, Jaffer Machano
amesema katika kutimiza wajibu wa TIB kama benki ya maendeleo, ujenzi wa
miundombinu umepewa kipaumbele na hii ni pamoja na miundombinu ya sekta
ya Mawasiliano.
“Kama alivyosema Dk. Kazaura, lengo la mpango mzima ni kuwapatia
Dola milioni 329 na TIB ipo tayari kuhakikisha mradi huu unafanikiwa kwa
kushirikisha kampuni zote za TIB group. Mfano mzuri ni mradi huu wa
kwanza ambao umefanywa na kampuni tanzu ya TIB group- TIB Corporate
Bank, amesema Jaffer Machano.”
Baadhi ya huduma za TTCL zitakazoimarika baada ya uwezeshaji huu
ni pamoja huduma za simu na intaneti yenye kasi kubwa inayowezesha
huduma za kijamii kufanyika kwa urahisi kwa njia ya mtandao. Huduma kama
vile za Elimu kwa njia ya mtandao (E education), Afya kwa njia ya
mtandao (E health) na huduma katika Sekta nyingine za kiuchumi kama vile
Biashara, Viwanda na Kilimo nazo zitanufaika sana ambapo
wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali watapata Mawasiliano
ya uhakika katika kufanikisha shughuli zao.
Kampuni ya Simu Tanzania TTCL ipo mbioni kuanzisha huduma ya
kusafirisha fedha kwa njia ya Mtandao ifikapo robo ya pili ya mwaka huu
ili kutekeleza ombi la muda mrefu la Wateja wake wanaohitaji sana
kuanzishwa kwa huduma hii kutokana na Mtandao mpana wa Kampuni
uliosambaa ndani na nje ya nchi na unafuu wa gharama.


No comments:
Post a Comment