Ndugu Waandishi wa Habari,
Ninapenda
kutoa taarifa kwa umma, kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu
ulioanza tarehe 15 Agosti, 2015 katika mkoa wa Dar es Salaam na kusambaa
kwa kasi katika Mikoa mingine 21 ya Tanzania Bara ambayo ni Pwani,
Morogoro, Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Kigoma, Geita, Mara, Manyara,
Arusha, Shinyanga, Tabora, Singida, Tanga, Lindi, Rukwa, Kagera, Katavi,
Mbeya na Mwanza na Simiyu.
Tangu ugonjwa huu uanze, jumla ya watu 12,810 wameugua Kipindupindu, na kati yao jumla ya watu 202 wameshafariki kwa ugonjwa huu ambayo ni sawa na asilimia 1.6 ya waliougua.
Katika
kipindi cha wiki iliyoanza tarehe 28 Desemba 2015 hadi tarehe 3 Januari
2016, kumekuwa na jumla ya wagonjwa walioripotiwa 590 na vifo 6, ambayo
ni asilimia 0.01 ya wagonjwa wote.
Mkoa
wa Mara (Musoma Mjini) ndio ulikuwa unaongoza kwa kasi ya maambukizi ya
ugonjwa wa kipindupindu ukifuatiwa na Singida (Iramba), Morogoro
(Morogoro Vijijini) na Manyara (Simanjiro).
Ndugu Waandishi wa Habari,
Takwimu
zinaonyesha kuwa licha ya kuwa na nafuu katika wiki ya nyuma, wiki hii
kasi ya maambukizi inaonesha kupanda tena kwenye mikoa ya Mwanza na
Arusha.
Katika
mkoa wa Arusha, maambukizi yamepanda kutoka wagonjwa wapya 60 hadi 111
kwa wiki. Katika mkoa wa Mwanza, kasi ya maambukizi imepanda kutoka
wagonjwa wapya 45 hadi 66 kwa wiki.
Kasi ya maambukizi ya Kipindupindu katika wiki iliyopita imepungua kwa kiasi kikubwa katika mikoa ya Mbeya na Tanga. Aidha, mikoa ya Dar-es-Salaam na Lindi haijaripoti mgonjwa yeyote mpya wa Kipindupindu katika wiki iliyopita.
Tunawapongeza
kwa hatua hii kutokana na juhudi zinazofanywa na wadau ambao kwa
pamoja, wameshirikiana kudhibiti ugonjwa huu kwa karibu zaidi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana
na Sekta nyingine husika, wadau wa maendeleo na wadau wengine inaendelea
kukabiliana na ugonjwa huu kwa njia mbalimbali.
Kikosi
kazi maalum chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kinakamilisha
mpango unaoshirikisha Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee
na Watoto , TAMISEMI, Wizara ya Maji na Umwagiliaji, DAWASCO, DAWASA,
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi pamoja na Sekretariat ya
Mkoa wa Dar-es-Salaam, kwa ajili ya kuhakikisha kuwa mikakati ya
kupambana na ugonjwa huu inakuwa jumuishi na ya haraka.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Bado
Wizara inaendelea kusisitiza kuwa, ili kudhibiti ugonjwa na kuokoa vifo
vinavyotokana na ugonjwa huu, wananchi wanasisitizwa kunywa maji yaliyo
safi na salama, kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira
yasiyo safi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji safi
yanayotiririka:-
- kabla na baada ya kula
- baada ya kutoka chooni
- baada ya kumnawisha mtoto aliyejisaidia
- baada ya kumhudumia mgonjwa
Aidha,
ni muhimu kuhakikisha kuwa wananchi wanatumia vyoo wakati wote na
kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, mabwawa na ziwani.
Wizara ilishapiga marufuku kuuza matunda yaliyokatwa na vyakula barabarani katika mazingira yasiyo safi na salama.
Hivyo,
Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji ambao ni Waganga
Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Maafisa Afya, ziendelee kutoa taarifa kuhusu
utekelezaji wa jambo hili.
Wizara
inapeleka tena timu za wataalm katika mikoa iliyoathirika zaidi na
kipindupindu ambayo ni Simiyu, Mara, Morogoro, Manyara, Singida, Arusha
na Mwanza. Timu hizi zitaungana na timu za mkoa wa wilaya kusaidia
kudhibiti ugonjwa huu.
Hitimisho
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea
kukumbusha kuwa, mikoa ambayo bado haijaathirika ichukue hatua za
tahadhari za kuzuia ili isipate mgonjwa yeyote wa Kipindupindu.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment