Simba avamia Kijijini na kuua wawili ( Baba na Mwana ) - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Thursday, 7 January 2016

Simba avamia Kijijini na kuua wawili ( Baba na Mwana )


WATU wawili, baba na mwanawe wamekufa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa na simba mkoani Katavi. 
Tukio hilo lilijiri Januari 3, mwaka huu, pale mkazi wa kijiji cha Sitalike wilayani Nsimbo Wilaya ya Mlele, John Jeremiah (45) na mwanawe mwenye umri wa miaka mitano, walipouawa na simba baada ya kuwavamia wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Anjelo alisema kuwa kutokana na mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi kutokuwa imara, simba huyo aliuparamia, akausukuma na kuingia ndani.

Inadaiwa kuwa simba huyo baada ya kumjeruhi vibaya na kumsababishia kifo Jeremiah alimvamia mtoto wake na kula kiwiliwili chake ambapo alibakiza kichwa kisha akaondoka na kutokomea porini. Kijiji cha Sitalike kinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo wilayani Mlele.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Anjelo alitoa taarifa kwa askari wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambapo walianza kumsaka simba huyo wakishirikiana na wananchi. Walifanikiwa kumuua simba huyo.

Inaelezwa kuwa baada ya kumuua simba huyo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walitaka wapewe mzoga wa mnyama huyo kwa ajili ya kitoweo huku wengine wakidai viungo vyake ni tiba za kijadi na mazindiko, lakini askari hao wa wanyama pori walikataa na kuondoka na mzoga wa mnyama huyo kwa madai kuwa wanenda kuuteketeza kwa moto.


Post a Comment