SERIKALI
inatarajia kutoa bei elekezi ya uuzaji wa ardhi, tofauti na hali ya
sasa ambayo viwanja vimekuwa vikiuzwa kwa bei ya juu na kufanya watu
wasio na uwezo kiuchumi kushindwa kumiliki na kujenga nyumba.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , Wiliam Lukuvi alisema jana
kwamba serikali inaandaa utaratibu wa kutoa bei hiyo elekezi,
itakayohusu watu wote.
Alitoa
taarifa hiyo jana mjini Kibaha katika mkoa wa Pwani, wakati alipofanya
ziara ya siku moja ya kutaka kufahamu kero mbalimbali zilizo kwenye
Idara ya Ardhi katika mkoa wa Pwani, zinazokabili wananchi.
Alisema
bei dira hiyo itakuwa kwa watu wote wanaouza ardhi kwa maana kwamba,
kabla ya kuuza, watatakiwa kuwasiliana na serikali ili wananchi
wapunguziwe kero ya kushindwa kumiliki ardhi kwa ajili ya shughuli
mbalimbali za maendeleo. Alisema ardhi ni huduma na si biashara.
Waziri
Lukuvi alisema baadhi ya watu wamefanya ardhi, kama ndiyo sehemu ya
kujinufaisha kwa kununua mashamba, kisha kuyagawa viwanja ambavyo
huviuza kwa bei kubwa. Alisema jambo hilo limekuwa likisababisha
wananchi wa kawaida, kushindwa kumudu kununua viwanja.
“Msifanye
ardhi kama biashara. Hii ni huduma na huduma haipaswi kutozwa gharama
kubwa. Utashangaa eneo kama Kibaha, kiwanja kinauzwa kiasi cha shilingi
milioni kumi. Kwa mtu wa hapa ana uwezo gani?” alisema.
Aliendelea kusema, “Kwa mfano, pale Kibada viwanja vilikuwa vikiuzwa kwa shilingi milioni tatu tu hatuwezi kukubali hali hii iendelee.”
Alisema
hata wale ambao wamewekeza ardhi kwa muda mrefu na kufanya kama rehani
kwa ajili ya kukopa fedha kwenye benki zao, wamekuwa ni tatizo kubwa.
Alieleza
kwamba, wengi wao wanaoomba mashamba makubwa serikalini, wamekuwa
wakibadili mashamba hayo na kuwa viwanja ambavyo huviuza kwa bei mbaya. “Na ni hao hao wanamiliki maeneo mbalimbali hapa nchini kwani majina ni yale yale,” alisema.
No comments:
Post a Comment