MSD Yajiandaa Kuanza Kuzalisha Dawa Nchini - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Tuesday, 12 January 2016

MSD Yajiandaa Kuanza Kuzalisha Dawa Nchini


BOHARI Kuu ya Dawa (MSD), imesema iko kwenye hatua nzuri za kuanzisha mradi wa uzalishaji dawa na vifaa tiba nchini kwa ubia na sekta binafsi, lengo likiwa kupunguza tatizo la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Mwanakunu alisema zabuni ya kumpata mtaalamu mshauri imekwishatangazwa na inategemea kukamilika mwezi huu.

Alisema, kwa sasa Bohari huagiza kutoka nje ya nchi dawa na vifaa tiba takribani asilimia 80 kutokana na uchache na uwezo mdogo wa viwanda vya ndani vya kuzalisha dawa na vifaa tiba.

Bwanakunu alisema, hali hiyo huilazimu MSD kuagiza bidhaa zake kwa wingi kukidhi mahitaji ya muda mrefu na hivyo kulazimika kuwa na sehemu kubwa ya kuhifadhia bidhaa hizo.

Akizungumzia uwekaji nembo kwenye dawa za serikali, Bwanakunu alisema katika mwaka wa fedha 2013/ 2014, MSD ilianza kuweka nembo ya GOT ikimaanisha Government of Tanzania (Serikali ya Tanzania).

Alisema, nembo hiyo imewekwa kwenye vidonge, vifaa tiba na vitendanishi vya maabara, kudhibiti kupelekwa kwenye maduka binafsi ya dawa, badala ya kutumiwa na walengwa ambao wanatibiwa katika hospitali zinazosambaziwa dawa na MSD.

“Awali, MSD ilikuwa ikiweka nembo ya MSD katika vifungashio tu, ambapo ilikuwa ni rahisi dawa hizo kuhujumiwa na kwenda kusikostahili. Kwa kuweka nembo hiyo ya GOT pamoja na MSD katika dawa, ni hatua mojawapo itakayosaidia kupunguza ama kudhibiti kabisa tatizo la wizi wa dawa za serikali,” Bwanakunu alisema.

Aliweka wazi kuwa hadi sasa asilimia 80 ya bidhaa zimekwishawekewa nembo ya GOT na kwamba wazabuni wengine wote wanaopata zabuni za kupeleka dawa kwenye bohari hiyo wanaelekezwa kuzingatia utaratibu huo wa kuweka nembo ya GOT na MSD.


“Kufikia Juni 2016 nembo ya MSD na GOT zitakuwa zimewekwa kwenye bidhaa zote,” alisema 
Post a Comment