Sarakasi Zaanza Tena Umeya Dar es Salaam - LEKULE

Breaking

23 Jan 2016

Sarakasi Zaanza Tena Umeya Dar es Salaam



HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam imeahirisha uchaguzi wa meya wa Jiji uliokuwa ufanyike leo, mpaka hapo tarehe itakapotangazwa baadaye.

Mkuu wa Kitengo cha Itifaki na Uhusiano na Umma wa Jiji, Gaston Makwembe alisema uchaguzi huo uliokuwa ufanyike leo saa nne asubuhi katika ukumbi wa Mmikutano wa Karimjee, umeahirishwa.

Alisema tarehe ya uchaguzi huo itapangwa baadaye na taarifa zitatolewa kwa wananchi kupitia vyombo vya habari bila kueleza sababu ya kuahirishwa kwa uchaguzi huo.

Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa na mvutano wa aina yake kati ya vyama vinavyounda na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Diwani wa Kata ya Vijibweni, Isaya Mwita (Chadema) ndiye atapeperusha bendera ya Ukawa huku mgombea wa nafasi ya Naibu Meya akitarajiwa kutoka CUF. Chama Cha Mapinduzi (CCM ) wakiwakilishwa na Diwani wa Kinondoni, Yusuph Omary Yenga.

Inaelezwa kuwa Ukawa wanapewa nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho kutokana na kuwa na idadi kubwa ya madiwani ambapo wanaizidi CCM kwa jumla ya madiwani 13.

Ikiwa Ukawa watafanikiwa kutwaa jiji hilo, itakuwa ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa wapinzani kuliongoza tangu kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992.

Awali, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene, alitoa mwito kwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia uchaguzi huo kwa amani na haki ili usifanyike kama wa kumtafuta meya wa Ilala na Kinondoni uliokuwa na mizengwe mingi.

No comments: