Ahukumiwa Miaka Mitano Jela Kwa Kuiba Mbuzi Mmoja - LEKULE

23 Jan 2016

Ahukumiwa Miaka Mitano Jela Kwa Kuiba Mbuzi Mmoja



MKAZI wa kitongoji cha Ilembo katika mji mdogo wa Vwawa wilayani Mbozi mkoani Mbeya, Patrick Moses (19) amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela baada ya kukutwa na hatia ya wizi wa mbuzi mmoja mwenye thamani ya Sh 85,000.

Hukumu hiyo imetolewa juzi na Mahakama ya Mwanzo Vwawa mjini, wilayani Mbozi ambapo Hakimu wa Mahakama hiyo, Lazima Mwaijage alisema ametoa hukumu hiyo kwa mujibu wa kifungu cha Sheria namba 268.

Awali imedaiwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa jeshi la polisi Hamis Mohamed kuwa mnamo Januari 20, mwaka huu saa 11 jioni mshitakiwa alivamia nyumbani kwa Bahati Mtafya (38) na kuiba mbuzi mmoja mwenye thamani ya shilingi 85,000 jambo ambalo ni kinyume na Sheria namba 229 sura ya 16 ya kanuni ya adhabu.

Kufuatia kosa hilo, Mwendesha Mashitaka huyo ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wale wenye nia ya kutenda kosa kama hilo kutokana na wimbi kubwa la vijana kujikita katika wizi na kuacha kufanya kazi zilizo halali.

Akijitetea kabla ya kutolewa kwa hukumu, mshitakiwa ambaye tangu awali alikiri kutenda kosa hilo, aliomba kupunguziwa adhabu akisema anategemewa na familia yake.

No comments: