Radi Yaua watu Watatu wa Familia moja Rufiji - LEKULE

Breaking

20 Jan 2016

Radi Yaua watu Watatu wa Familia moja Rufiji



Watu watatu wa familia moja, wakazi wa Kijiji cha Mchukwi wilayani hapa Mkoa wa Pwani, wamekufa baada ya kupigwa na radi jikoni wakati mvua zikinyesha.

Tukio hilo limetokea  jana jioni katika kijiji hicho. Inadaiwa kuwa radi hiyo ilianza kupiga mti uliokuwa pembezoni mwa jiko hilo kabla ya kuwaua ndugu hao.

Shuhuda wa tukio hilo, Amina Tenge ambaye pia ni Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, alisema waliwachukua ndugu hao na kuwapeleka Hospitali ya Misheni ya Mchukwi kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya majeraha waliyopata.

“Tulipofika hospitali walikuwa wameshafariki tayari,” alisema Tenge.

Mganga wa zamu wa Hospital hiyo, Esther Mtini aliwataja marehemu hao kuwa ni Desteria Simba (40), Deborah Simba (2) na Amani Matimbwa (6).

Alisema baada ya kuifanyia uchunguzi miili hiyo, walibaini kuwa Desteria alikuwa ameungua kifuani, tumboni na shavuni.

“Amani aliungua tumboni na katika sehemu zake za siri na Deborah hakuwa na jeraha lolote,” alisema Dk Mtini.

Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Nurdin Babu aliwataka wananchi kuepuka kukaa chini ya miti au karibu na miti katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha kwani ni hatari kwa maisha yao.

“Mvua hizi zinazoendelea kunyesha sasa zina madhara kwa sababu zinaambatana na radi na upepo mkali, lazima tuchukue tahadhari kwa kuacha kukaa chini ya miti au jirani ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea,” alisema Babu.

Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), juzi ilitoa tahadhari ya kuwapo kwa mvua kubwa zinazoambatana na radi katika baadhi ya mikoa nchini, ukiwamo Pwani.    

No comments: