Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange
Mtoto
mwenye umri wa miaka 13 anayesoma darasa la sita katika Shule ya Msingi
Wishiteleja wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga, ameozeshwa kwa nguvu na
wazazi wake baada ya kupokea mahari ya ng’ombe 13.
Akizungumza
na waandishi wa habari mjini Shinyanga juzi, Mkurugenzi wa Shirika la
AGAPE, John Myola alisema mwanafunzi huyo alifungishwa ndoa ya kimila
Septemba 25, mwaka jana katika Kitongoji cha Nyamikoma Kijiji cha
Buchambi wilayani Kishapu.
Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Mika Nyange alisema hakuwa na taarifa
kuhusu tukio hilo na aliahidi kuwasiliana na Mkuu wa Polisi wilayani
Kishapu, ampatie taarifa kamili aitoe rasmi kwa waandishi wa habari.
Hata hivyo,alipotafutwa Mkuu
wa Wilaya ya Kishapu, Hawa Ngh’umbi alikiri kupokea nakala ya barua
kutoka Agape iliyozungumzia juu ya kufungishwa ndoa kwa mtoto huyo.
Alikemea kitendo hicho na kuahidi kumsaka mtuhumiwa akamatwe na kufikishwa mahakamani.
Kwa
mujibu wa Mkuu wa Shirika la Agape, Myola, siku ya tukio, ofisi yake
ilipokea taarifa kutoka kwa wasamaria wema ambao walieleza kusikitishwa
na kitendo cha mtoto huyo mdogo, kuozeshwa kinyume cha sheria za nchi na
kudai kuwa zipo shutuma za viongozi wa serikali ya kijiji na kitongoji
kushiriki.
Alisema
baada ya kupokea taarifa hizo, alikwenda katika eneo la tukio
akiongozana na polisi kutoka kituo kidogo cha Maganzo wilayani Kishapu,
ambapo walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa na viongozi wa serikali ya
kitongoji na kijiji, waliodaiwa kuhusika katika suala la kupatanisha
mahari.
Mwanamume
aliyekuwa akifunga ndoa na mwanafunzi huyo, alitajwa kwa jina la
Emmanuel Njile, mkazi wa Kijiji cha Isemelo Wilaya ya Igunga mkoani
Tabora, ambaye alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi, alikofunguliwa
jalada la kesi namba RB/ MGZ/495/2015 na kuwekwa mahabusu.
Alidai
kuwa baada ya kusambaratisha ndoa hiyo, walipewa fomu namba tatu (PF.
3) ili wampeleke mtoto huyo hospitali, ambako alifanyiwa vipimo na
daktari, ambako hata hivyo inadaiwa ilibainika hakuwa ameingiliwa
kimwili.
Alisema
siku mbili baadaye, Septemba 27, 2015 usiku saa 2, walipokea taarifa za
kuwepo kwa kikao cha siri katika baa moja ya mjini Maganzo,
kilichowahusisha baadhi ya viongozi na watendaji (wakiwemo polisi)
waliokutana na kaka wa mtoto, wakijadili jambo ambalo haikufahamika ni
nini.
“Kwa
kweli tulipata wasiwasi juu ya kikao hicho cha usiku, tuliamini kuna
mpango mchafu ulikuwa ukifanyika, na kweli asubuhi yake, Septemba 28,
2015, tulielezwa kuwa mtuhumiwa alikuwa ametolewa mahabusu na kuruhusiwa
kurudi nyumbani, ambako alimchukua mtoto aliyeozeshwa na kuondoka naye.
“Tulifuatilia
na kuelezwa kuwa amekwenda kwao Kijiji cha Isemelo wilayani Igunga Mkoa
wa Tabora ambako hivi sasa wanaishi kama mke na mume.Tulimwandikia
barua Mkuu wa Polisi wilayani Kishapu ili kupata ufafanuzi juu ya kesi
hiyo".
Akifafanua
kwamba, katika barua iliyotoka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kishapu
yenye Kumb. Na. A.20/08/ Vol.1/13 ya Desemba 14, 2015, mtuhumiwa
aliyetajwa kuhusika na kesi iliyofunguliwa kwa jalada namba RB/
MGZ/495/2015 alikuwa ni Daudi Sagi badala ya Emmanuel Njile, hatua
ambayo alisema walishangaa.
No comments:
Post a Comment