Mtibwa Sugar yakubali kuendelea kuwa teja wa Azam FC - LEKULE BLOG

Breaking

Header Ads

Sunday, 3 January 2016

Mtibwa Sugar yakubali kuendelea kuwa teja wa Azam FC

Hussein Javu akishangilia goli aliloifungia Mtibwa
Hussein Javu akishangilia goli aliloifungia Mtibwa
Mchezo kati ya Azam vs Mtibwa Sugar umemalizika kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana kwa goli 1-1 kwenye mchezo wa pili wa Mapinduzi Cup ulionza majira ya saa 2:15 usiku na timu hizo kugawana pointi mojamoja.
Mtibwa Sugar waliandika goli lao dakika ya 61 kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wao Hussein Javu aliyerejea kwenye timu yake ya zamani mara baada ya kutemwa na kikosi cha Yanga. Javu alifunga goli hilo akimalizia pasi ya Kichuya ambaye aliunasa mpira kutokana na makosa ya mlinzi wa Azam FC Said Mourad.
Dakika ya 74 nahodha wa Azam FC John Bocco ‘Adebayor’ aliisawazishia timu yake kwa mkwaju wa penati baada ya yeye mwenyewe kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari la Mtibwa Sugar.
Kama kawaida inapopigwa mechi kati ya Azam FC vs Mtibwa Sugar huwa ni zaidi ya fainali, timu hizi zimekuwa na upinzani mkubwa sana. Kabla ya kukutana kwenye mchezo wa leo timu hizi zilikutana kwenye mchezo wa ligi kuu Tanzania bara uliopigwa Jumatano iliyopita kwenye uwanja wa Azam Complex na Azam kupata ushindi wa goli 1-0 na kufanikiwa kuongoza ligi.
Kwenye mchezo wa leo, Mtibwa waliwashika vilivyo Azam na kuwaweka ‘mfukoni’ huku wakisukuma mpira wa haraka na kuliweka lango la Azam kwenye presha kwa muda wote wa kipindi cha kwanza na kipindi cha pili. Unaweza ukasema Mtibwa wamekuwa hawawezi kucheza na nafasi kutokana na kupoteza nafasi ambazo wamekuwa wakizitengeneza.
Wakati mchezo huo ukielekea ukingoni, Mtibwa walipata bao la pili lakini mwamuzi wa mchezo alilikataa kwa madai kwamba mfungaji alikuwa ameotea. Kukataliwa kwa goli hilo kulizua ‘mtiti’ kwa mshika kibendera ambaye ndiye alinyoosha kibendera kuashiria mfungaji aliotea.

Lakini baada ya kumalizika kwa mchezo ilibidi waamuzi watolewe kwa msaada wa ulinzi mkali wa polisi kutokana na wachezaji na benchi zima la ufundi la Mtibwa Sugar kuwazonga waamuzi hao.
Post a Comment