Mkuu wa Oganaizesheni wa NCCR-Mageuzi Amtaka LOWASSA Ajieleze Kama Ataendelea Kubaki CHADEMA Iwapo Jina lake Litaenguliwa Mbio za Urais 2020 - LEKULE

Breaking

21 Jan 2016

Mkuu wa Oganaizesheni wa NCCR-Mageuzi Amtaka LOWASSA Ajieleze Kama Ataendelea Kubaki CHADEMA Iwapo Jina lake Litaenguliwa Mbio za Urais 2020


Kufuatia  kauli ya aliyekuwa mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa ya kugombea tena urais mwaka 2020, Mkuu wa Oganaizesheni wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura amemhoji Lowassa kama atakuwa tayari kuendelea kutumikia Ukawa kama jina lake halitapendekezwa kugombea nafasi hiyo.
Sungura amesema kauli hiyo ya Lowassa kupambana tena katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2020 kunategemea maamuzi ya chama kupitisha jina lake.

“Nimemsikia Lowassa anasema kuwa anajiandaa kupambana na Rais John Magufuli mwaka 2020, lakini je, yuko tayari kuheshimu maamuzi ya chama kwa maslahi ya wakati huo?” Alihoji Sungura.

Sungura alisema mwaka jana jina la Lowassa lilipochujwa kwenye wagombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alijiondoa na kuhamia Chadema.

“Je, atakuwa tayari kuheshimu maamuzi ya chama pale ambapo jina lake halitapitishwa kugombea urais Chadema au atahamia chama chake?” Alihoji Sungura.

Akizungumzia ushindi wa viti vya meya uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Sungura alisema ushindi huo ambao wameshinda wagombea wa Chadema na CUF usitafsiriwe kuwa ni ushindi wa Ukawa, bali ni ushindi wa Chadema na CUF .

“Nasema hayo kwa sababu ukizungumzia Ukawa unazungumzia vyama vinne ambavyo ni Chadema, NCCR Mageuzi, NLD na CUF, lakini kilichofanyika kuna baadhi ya kata tulisimamisha wagombea lakini walituwekea kauzibe tusipate,” alisema Sungura.


Sungura alisema baadhi ya vyama ndani ya Ukawa wana ubinafsi kuwachanganya watanzania kwa neno Ukawa ambalo halina maana yoyote badala yake kuviua vyama vingine ndani ya umoja huo.

No comments: