Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Ashinda kesi ya Uchaguzi dhidi ya Kippi Warioba - LEKULE

Breaking

16 Jan 2016

Mbunge wa Kawe Halima Mdee, Ashinda kesi ya Uchaguzi dhidi ya Kippi Warioba


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imefuta kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge, iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kippi Warioba, dhidi ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Jaji Zainabu Mruke alitoa uamuzi huo jana, kwa kuwa Warioba aliomba kuondoa shauri hilo mahakamani baada ya kukubali hoja za pingamizi la awali zilizowasilishwa na Mdee pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Warioba alifungua kesi ya uchaguzi akipinga matokeo yaliyompa udhindi Mdee, dhidi Mwasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni pamoja na Mdee.

Katika kesi hiyo namba 7 ya mwaka 2015, Warioba alikuwa akiiomba mahakama hiyo ibatilishe matokeo ya uchaguzi huo pamoja na mambo mengine, kwa kuwa haukuwa huru na wa haki.

Hata hivyo, Mdee pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliwasilisha, pingamizi la awali, wakiomba mahakama itupilie mbali kesi hiyo, lakini wakati wa kusikiliza pingamizi, Warioba kupitia, wakili wake Emmanuel Makene alikubaliana na hoja za pingamizi hilo na kuomba mahakama iondoe kesi hiyo.


Akitoa uamuzi jana, Jaji Mruke alisema, kwa kuwa mdai amekubali hoja za pingamizi na ameamua kuiondoa mahakamani kesi hiyo, basi mahakama inaamuru kesi iondolewa.

No comments: