SERIKALI
imeendelea kuisafisha Bandari kwa kuwaondoa watendaji wa ngazi za juu
na kuwahamishia wizarani ili kuongeza ufanisi katika utendaji, sambamba
na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Wakati hayo yakitokea Bandari, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) amesimamishwa kazi huku Mhasibu Mkuu na Meneja Manunuzi wa taasisi hiyo wakihamishwa kwa tuhuma za kushindwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika taasisi hiyo.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu mabadiliko
Bandarini, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame
Mbarawa (pichani) alisema serikali ya awamu ya tano imedhamiria
kuhakikisha inasimamia mapato ya serikali na taasisi zinafanya kazi kwa
ufanisi mkubwa.
Aliwataja watumishi
walioondolewa Bandari kuwa ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu,
Peter Gawile, Kaimu Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA), Killian Challe na Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi, Mashaka
Kishanda.
Alisema
watendaji hao wamerudishwa wizarani na itafanyika tathmini ili
waangaliwe watapangiwa nafasi gani kwa kuwa inawezekana katika Bandari
uwezo wao na ufanisi wao ulikuwa mdogo ila inawezekana maeneo mengine
wakafanya vizuri zaidi.
Aidha
alisema imewateua watendaji wengine kushika nafasi hizo akiwemo Anthony
Mbilinyi kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambaye anakwenda
Bandari kushika nafasi ya Gawile, Benito Kalinga ambaye alikuwa Ofisa
Manunuzi Mkuu wa TCRA anayeenda Bandari kushika nafasi ya Kishanda na
Abdulrahaman Bamba ambae alikuwa TEHAMA Uchukuzi anayeenda kushika
nafasi ya Challe.
“Tatizo
kubwa lililokuwa linaonekana pale Bandari ni mfumo wa IT hivyo tumeamua
hao waondoke… Tunaamini tukiwapa ushirikiano watendaji hawa wanaoingia
watafanya vizuri zaidi na kufanikisha azma ya serikali ya kuongeza
ukusanyaji wa mapato,” alisema.
Katika
hatua nyingine, Profesa Mbarawa amemsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Charles Chacha na kutaka
kuhamishwa mara moja kwa Mhasibu Mkuu Alhaji Said Mteule na Meneja
manunuzi wa taasisi hiyo, Said Kaswela kwa kushindwa kusimamia
ukusanyaji wa mapato katika taasisi hiyo.
Serikali
pia imeona ifanye uchunguzi kuhusu ununuzi wa mtambo wa kufuatilia
vyombo angani unaojulikana kama Automatic Data Surveillance-Broadcast
(ADS-B) na mtambo wa kukusanya taarifa za usafiri wa anga (AMHS), ambayo
imegharimu kiasi cha Euro milioni 1.5.
Mbarawa
alitoa agizo hilo jana akiwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip
Mpango pamoja na watendaji wa TCAA katika ziara aliyoizungumzia kuwa ni
ya kuangalia uendeshaji na ukusanyaji wa mapato unavyofanyika katika
taasisi hiyo.
Waziri
huyo alisema kuna mambo yamejitokeza hivyo serikali imeona lazima
ifanye uchunguzi kwenye ununuzi wa baadhi ya mitambo na pia imebaini
kuna upotevu mkubwa wa ukusanyaji wa mapato ambao umechangiwa na uongozi
wa taasisi kwa kutojipanga vizuri.
“Wizara
imeamua Chacha kuanzia leo (jana), hataendelea na nafasi hiyo tena
badala yake atatafutwa mwingine. Mhasibu Mkuu wa taasisi hii atahamishwa
na ofisa wa manunuzi wa taasisi hii. Iko haja ya kumpeleka sehemu
nyingine ili tupate mtu safi na makini,” alisema Waziri huyo.
Mitambo hiyo ilitakiwa kuanza kufanya kazi tangu Novemba mwaka jana, lakini mpaka sasa haijaanza kufanya kazi.
“Bora ubaki na watu wawili kwenye kazi kuliko 10 ambao sio waadilifu,” alisema Mbarawa.
Kwa
upande wake Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mpango alisema kikubwa
wanachopigania ni kuhakikisha serikali inakusanya mapato yote ya kodi na
yasiyo ya kodi na kuongeza kuwa taasisi hiyo ina vyanzo ambavyo
vingeweza kuingizia serikali fedha nyingi.
“Mkaguzi
Mkuu alikuja na kufanya utafiti lakini taarifa aliyoitoa haikufanyiwa
kazi. Pia katika kudodosa inajulikana TCAA ina akaunti saba ambazo
zinatia shaka,”alisema Waziri Mpango na kuagiza akaunti hizo kutokuguswa mpaka uchunguzi utakapofanyika.
“Nimeagiza
ili fedha za taasisi hii zibaki salama isitoke hata senti, pia ndani ya
wiki mbili ufanyike ukaguzi kubaini upotevu wote wa fedha za umma
uliofanyika,” alisema na kuitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya
Umma (PPRA), ifanye uchunguzi wa mchakato mzima wa ununuzi wa mitambo
hiyo miwili ya ADSB na AMHS, pamoja na kusisitiza kuwa watumishi
waliosimamishwa watahamishwa mara moja.
No comments:
Post a Comment