MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi imezuia nyumba anayoishi Mchungaji wa
Kanisa la Assemblies of God Mikocheni, Dk. Getrude Lwakatare
kubomolewa.
Uamuzi huo wa mahakama ulitolewa juzi na Jaji John Mgeta, baada ya
Wakili wa Lwakatare, Emmanuel Muga kuwasilisha maombi ya kupinga
ubomoaji huo chini ya hati ya dharura.
Jaji Mgeta alizuia ubomoaji wa jengo hilo ama kuchukua hatua yoyote kuhusu jengo hilo lililopo Kawe Beach.
Muga aliwasilisha maombi akimwakilisha mdai ambaye ni mtoto wa
Mchungaji Lwakatare, Robert Brighton dhidi ya wadaiwa NEMC, Manispaa ya
Kinondoni na wadau wengine wote.
“Mheshimiwa jaji, nawasilisha maombi ya zuio la kubomoa nyumba ya
mteja wangu chini ya kifungu namba 95 cha Sheria ya Mwenendo wa Madai na
kifungu namba 2(3) cha JALA vinavyotoa mamlaka kwa mahakama kutoa nafuu
stahili pale kunapokuwa na ukiukwaji wa kuvunja haki ya wazi,” alidai.
Akitoa uamuzi huo alisema tayari pande husika zilikuwa na kesi namba
70 ya mwaka 2012 na ikamalizika kwa kutoa hukumu na kukazia hukumu
iliyompa haki ya ushindi mdai.
“Mahakama ilimpa haki mdai, lakini chakushangaza mdaiwa anakiuka
matakwa ya hukumu na kutaka kubomoa nyumba, kwa hali isiyokuwa ya
kawaida mdai anahitaji ulinzi wa mahakama hii ya haki,”alisema Jaji
Mgeta.
Alisema nyumba hiyo ipo katika kiwanja namba 2019 na 2020 ambapo hati yake ilitolewa mwaka 1979.
Inadaiwa mwaka 2011 NEMC ilitoa notisi ya kuvunja nyumba hiyo baada
ya kushinikizwa na wakazi wa eneo hilo wakidai ujenzi wake unaziba Mto
Ndumbwi na uko jirani na mikoko.
Wakili Muga aliwasilisha maombi ya kuzuia nyumba ya mteja wake
kubomolewa baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia wakala
wa misitu Tanzania (TFS ), kuweka alama ya X wakidai imo katika
hifadhi ya bahari.
No comments:
Post a Comment