Magufuli afuta hati ya hekta 1,870 Kapunga - LEKULE

Breaking

5 Jan 2016

Magufuli afuta hati ya hekta 1,870 Kapunga


Rais John Magufuli amemaliza mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kapunga Rice Project Limited na sasa hekta 1,780 zitakuwa mali ya wananchi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza jana katika mkutano wa hadhara ambao licha ya mvua kubwa, wananchi walimsikiliza kwa makini na kushangilia baada ya kupokea taarifa hiyo. Kijiji cha Kapunga kina wananchi 4,500.
Lukuvi alisema hatua hiyo ni zawadi ya kwanza ya Rais kwa wananchi Tanzania kwa kutatua mgogoro wa siku nyingi.
“Rais amedhamiria kuwasaidia wananchi, hivyo naomba (Mkuu wa Mkoa), uandae orodha ya watu wote wanaomiliki mashamba yasiyoendelezwa ingawa wanapata mikopo kupitia hati za mashamba hayo ili kazi ya Serikali kuwapatia maeneo ya kulima na wananchi wa kawaida iweze kufanikiwa,” alisema.
Lukuvi alikwenda kwenye kijiji hicho kutangaza jambo ambalo aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka alilishindwa Januari 7, 2013.
Meneja wa Mradi Kapunga Rice Project, Sumil Tayic alisema viongozi wake wameafiki uamuzi wa Rais bila kinyongo na sasa wataimarisha ushirikiano mzuri na wananchi.
Mwakilishi wa wananchi, Sekela Sandube aliishukuru Serikali hususan Rais Magufuli na Waziri Lukuvi kwa kumaliza mgogoro ambao uliwashinda wengi kwa sababu za roho mbaya.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kapunga, Brighton Mwinuka alisema hatua ya Rais Magufuli kuwapatia eneo hilo kutakifanya kijiji kiwe na mipango ya maendeleo.
Kabla ya kwenda wilayani Mbarali jana, Lukuvi alikutana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kuanzia saa 2.24 hadi saa 3.57 kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Habari kutoka kwenye kikao hicho zilisema waziri aliwaeleza kinagaubaga kuhusu msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua kero za wananchi na kwamba lazima viongozi wote wabadilike kiutendaji.
Alipoulizwa kilichozungumzwa Waziri Lukuvi alisema yalizungumzwa mambo mengi ya kiutendaji na baadhi angeyatoa Kapunga.
Mgogoro wa Kapunga
Mwaka 1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Kampuni ya Taifa ya Kilimo (Nafco), huku eneo la hekta 1,870 likiwa la wakulima wa kawaida.
Lakini katika mazingira ya kutatanisha, Serikali ilichukua hati moja iliyojumuisha hekta 5,500 na nyingine 1,870 bila kuwajulisha wananchi, hivyo mwekezaji aliponunua eneo la Nafco alikabidhiwa hati ya eneo lote.
Serikali ilibaini kwamba Nafco ilisajili na kupata hati moja kwa eneo lote likiwamo la kijiji lakini kwa miaka yote imeshindwa kutoa uamuzi.
Mwaka 2013, mwekezaji huyo alidaiwa kumwaga sumu kwenye mashamba ya mpunga yaliyokuwa na mgogoro na Serikali ilimtuma Profesa Tibaijuka kuulimaliza.
Alifika akiwa na msimamo wa kutaka kumshauri Rais wa Awamu ya Nne afute hati ya eneo linalozidi ambalo ni hekta 1,870, lakini baada ya kupata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji, Justin Vermaak alisema anawashangaa wananchi kudai kwa nguvu eneo ambalo ni la mwekezaji kisheria.

“Baada ya kuzunguka nimeona mwekezaji hana matatizo, chanzo cha mgogoro ni Serikali, hivyo itaendelea kuzungumza na mwekezaji na wananchi ili kumaliza mgogoro,” alisema.

No comments: