CUF Wakutana Kujadili Kurudiwa Uchaguzi Zanzibar - LEKULE

Breaking

24 Jan 2016

CUF Wakutana Kujadili Kurudiwa Uchaguzi Zanzibar



CHAMA cha Wananchi CUF kimeitisha vikao vya juu vya kitaifa vya Chama ili kujadili marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliotangazwa kurudiwa Machi 20, 2016 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa, imesema kuwa vikao hivyo vitafanyika Januari 27 na 28 mwaka huu, na ndivyo vitakavyotoa msimamo rasmi wa CUF.

Ifuatayo ni taarifa kamili ya Jussa.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kufuatia tangazo jengine la kihuni lisilozingatia Katiba wala Sheria la Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha kutangaza tarehe 20 Machi, 2016 kwamba ni siku ya kile anachokiita uchaguzi wa marudio Zanzibar, Chama Cha Wananchi (CUF) kimeitisha vikao vya juu vya kitaifa vya Chama ili kujadili suala hilo na kutoa msimamo rasmi wa Chama.

Kamati ya Utendaji ya Taifa itakutana Jumatano, tarehe 27 Januari, 2016 na kufuatiwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa litakalokutana Alhamis, tarehe 28 Januari, 2016. Vikao hivyo vitafanyika Ofisi Kuu ya Chama, mjini Dar es Salaam.

Chama kinatoa wito na kuwanasihi Wazanzibari wote waliochoshwa na utawala wa kibabe na wa kidikteta wa CCM na ambao walikikataa chama hicho kwa kishindo tarehe 25 Oktoba, 2015 kuendelea kutunza amani na kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kusubiri maamuzi ya chama chao wanachokiamini.

HAKI SAWA KWA WOTE
ISMAIL JUSSA
KAIMU MKURUGENZI WA HABARI NA MAWASILIANO

No comments: