WIZARA YA FEDHA YAADHIMISHA SHEREHE ZA UHURU KWA KUFANYA USAFI - LEKULE

Breaking

10 Dec 2015

WIZARA YA FEDHA YAADHIMISHA SHEREHE ZA UHURU KWA KUFANYA USAFI


Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (wa tatu kulia) akielekea eneo la kufanya usafi kuzunguka maeneo ya ofisi za wizara hiyo leo jijini Dar es salaam ikiwa ni mwitikio na utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kufanya usafi katika eneo ya kazi wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru mwaka huu.
Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (DHRM) Wizara ya Fedha Deodata Makani akitoa maelekezo ya kufanya usafi kuzunguka ofisi za Wizara hiyo leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya watumishi wakikata matawi ya miti kwa makini bila kuharibu nya za simu yaliyokuwa kizuizi katika barabara eneo la ofisi za wizara ya fedha kwa lengo la kufanya usafi leo jijini Dar es salaam.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile akiendelea kufanya usafi katika moja ya sehem ya kuzunguka maeneo ya ofisi za wizara hiyo leo jijini Dar es salaam ikiwa ni mwitikio na utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kufanya usafi katika eneo ya kazi wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile akiongea na watumishi wa wizara hiyo leo jijini Dar es salaam mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi ikiwa ni mwitikio na utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kufanya usafi katika eneo ya kazi wakati wa maadhimisho ya sherehe za Uhuru mwaka huu.
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile leo ameiongoza wizara hiyo katika kuitikia na kutekeleza agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli la kufanya usafi katika eneo lao la kazi katika maadhimisho ya sherehe za Uhuru ya mwaka huu.

Akiongea na watumishi wa Wizara hiyo, Dkt. Likwelile alisema kuwa maadhimisho ya siku ya uhuru yaendelee kutumika kama kichocheo cha kujenga tabia ya kufanya kazi ikizingatiwa dhana iliyokuwepo tangu uhuru ilikuwa “Uhuru na Kazi” ambapo kwa sasa kaulimbiu ya Rais Dkt. Magufuli inasema “Hapa Kazi Tu”

“Ni uamuzi mzuri wa Rais, ni wa busara na unaendana na tulipotoka ambapo Tanzania inaamini katika “Uhuru na Kazi”, huu ni mwanzo wa kusimama kwa miguu yetu wenyewe ili kujiletea maendeleo kwa kuendelea kuwapiga vita maadui watatu wa taifa” alisema Dkt. Likwelile.

Dkt. Likwelile aliwataja maadui hao kuwa ni ujinga, maradhi na umasikini ambao ndiyo wamekuwa chanzo cha kurudisha nyuma juhudi za maendeleo, kwa kuimarisha suala la usafi katika mazingira yote nchini, itakuwa mwanzo wa kupambana na suala magonjwa milipuko ikiwemo kipindupindu ambao asili yake ni uchafu.

Aidha, Dkt. Likwelile aliwaasa watumishi wa wizara hiyo na Watanzanaia kwa ujumla kuenzi kazi iliyonzishwa na Mhe. Rais Dkt. Magufuli ya kufanya usafi na zoezi hilo liwe endelevu na la kudumu ambapo ameahidi kuwa wizara yake itapanga siku ya kufanya usafi mara kwa mara katika maeneo ya kazi ili kudumisha usafi ambao ni suala muhimu katika kuimarisha afya zao na ikizingatiwa watumishi hutumia muda mwingi wakiwa katika maeneo ya kazini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu (DHRM) Wizara ya Fedha Deodata Makani alisema kuwa mwitikio wa watumishi katika zoezi la usafi umekuwa mkubwa na wanapendekeza zoezi hilo liwe endelevu maana watumishi hutumia muda mwingi katika maeneo ya kazini hivyo ni vema kuyaweka mazingira hayo katika hali ya usafi ili yawe rafiki wakati wote wa kutekeleza majukumu yao. 

Naye mmoja wa watumishi wa Wizara hiyo William Muhoja alisema kuwa zoezi la kufanya usafi katika maeneo ya kazi linatakiwa kufanywa kila wakati ambapo itakuwa ni sehemu ya watumishi kuwajibika kwa jamii katika maeneo yao wanapoishi na wanapofanya kazi.

Sherehe za uhuru mwaka huu nchini zimeadhimishwa kwa namna tofauti na ilivyozoeleka miaka iliyopita ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mamlaka aliyonayo kikatiba alitangaza maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri ya 9 Disemba mwaka huu, Watanzania wote waitumie kwa kufanya kazi mbalimbali kama vile, mashambani, maofisini, sokoni, viwandani na usafi wa miji yao katika kutimiza dhana ya Uhuru na Kazi kwa vitendo.


Maadhimisho hayo yanaendelea nchi nzima ambapo kila halmashauri inatekeleza agizo la Mhe. Rais kwa vitendo kwa kufanya usafi katika maeneo yao, zoezi linashirikisha Wizara, idara, taasisi za Kiserikali na zisizo za kiserikali, maeneo ya viwanda, shule, vyuo, maeneo ya biashara, masoko na kuzunguka maeneo yote ya makazi ya watu.

No comments: