Rais
Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete pamoja na
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Welle Ndikilo wakielekea soko kuu la
Chalinze kushirikiana na wananchi kufanya usafi wa mazingira leo Desemba
9, 2015 ikiwa ni kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na
Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli
Rais
Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifanya
usafi katika soko kuu la Chalinze leo Desemba 9, 2015 ikiwa ni
kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na Rais Dkt John Pombe
Joseph Magufuli
Rais
Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakifanya
usafi katika soko kuu la Chalinze leo Desemba 9, 2015 ikiwa ni
kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa na Rais Dkt John Pombe
Joseph Magufuli
Rais
Mstaafu Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na wananchi wa Chalinze baada ya
kushirikiana nao kufanya usafi wa mazingira ya soko kuu la Chalinze leo
Desemba 9, 2015 ikiwa ni kuadhimisha miaka 54 ya UHURU kama ilivyoagizwa
na Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli.
RAIS
mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, amesema katika uongozi wake wa
miaka 10, hakuwahi kuagiza mtu asamehewe kontena lake lisilipe kodi na
angefanya hivyo, mapato ya Serikali yasingeongezeka kutoka Sh bilioni
177 kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.
Akizungumza
baada ya kuwashitukiza wananchi wa Chalinze katika Soko Kuu la eneo
hilo kwa kuungana nao kufanya usafi kuitikia agizo la Rais John Magufuli
jana asubuhi, Kikwete alisema katika uongozi wake hakuwahi kuagiza mtu
anayestahili kulipa kodi asilipe kodi.
Amesema
wakati huu ambao amepumzika baada ya kustaafu, amepata nafasi ya kusoma
mitandao na magazeti mbalimbali na kukuta baadhi ya watu wakimshutumu
na kumtukana yeye na familia yake wakimuhusisha na ukwepaji kodi.
“Ni
afadhali wanishambulie mimi ila wamuache Rais Magufuli (John Pombe)
afanye kazi, ni maneno ya walioshindwa wasinilaumu, aliyewashinda ni
Magufuli sasa hawana la kusema. Ni sawa na siasa za maji taka lakini
watakuwa wanapoteza muda wao na kufanya kazi bure, kwa kuwa mimi
sigombei kitu chochote tena.
“Wanahusisha
mpaka na familia yangu, kama mimi mwenyewe sijawahi kuruhusu mtu hata
mmoja atoe kontena bila kulipia kodi, siamini kama mke wangu (Mama
Salma) au mwanangu Ridhiwani (Mbunge wa Chalinze), wengeweza kufanya
hivyo tu na watu wakawasikiliza.
“Wanachonga
tuu, wengine wamesema Kikwete hachomoi, kwani nimechomeka nini?”
Alihoji na kusababisha watu walioshirikiana naye kufanya usafi katika
soko hilo kucheka na kuanza kushangilia.
Alisema
nafasi ya urais aliyoaminiwa na Watanzania kwa miaka kumi, ilikua yake
na haikuwa na ubia na mkewe wala mtu mwingine yeyote.
Kikwete
aliwataka Watanzania wamuunge mkono Rais Magufuli katika jitihada
anazofanya za kukabiliana na wakwepa kodi, huku akitoa mfano akisema
wakwepa kodi kwa Serikali ni kama inzi na kidonda, hawaondoki bila
kufukuzwa na ukiacha kuwafukuza wanarudi.
Aliwakumbusha
wananchi kwamba Serikali ina wajibu wa kutumikia wananchi katika
mahitaji yao, ambayo utekelezaji wake unahitaji fedha.
“Serikali
ina wajibu kwa wananchi, wanataka barabara, shule, hospitali ziwe na
dawa na mengine mengi, lakini haya yote yanahitaji fedha na Serikali
inapata fedha kutoka katika vyanzo vya kodi,” alisema.
Alisema
pia yapo mapato mengine ikiwemo ushuru mbalimbali kama katika kulipia
leseni, hati za kusafiria na nyingine, lakini pia Serikali inaweza
kuchukua mikopo na misaada.
Hata
hivyo alisema Serikali inapaswa kuimarisha ukusanyaji wa mapato hasa ya
kodi, ikiwemo kodi ya mapato na ushuru wa forodha na hayo ya mikopo na
misaada, yanatakiwa iwe sehemu ndogo ya mapato ya Serikali.
Kikwete
alisisitiza yeye wakati wa uongozi wake kazi hiyo ya kuongeza
ukusanyaji wa mapato na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ilifanyika,
ndio maana akafanikiwa kuongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh bilioni 177
kwa mwezi mpaka Sh bilioni 900.
Pamoja
na mafanikio hayo ya uongozi wake, Kikwete alisema bado mahitaji ya
Serikali kwa watu wake yameendelea kuwa makubwa, kuliko upatikanaji wa
mapato.
“Tunapaswa
kuendelea kuboresha mifumo ya kodi, taasisi za mapato na kupata
watendaji waadilifu, kwa kuwa kama mifumo na taasisi vikiwa imara,
lakini watendaji si waaminifu haisaidii.
“Hajazaliwa
mtu anayependa kulipa kodi, ndio maana wanaokwepa kodi wanatumia uzembe
wa watendaji na wengine wanatumia rushwa…sasa uzembe na ulaji wa rushwa
lazima tupige vita na hiyo ndiyo kazi anayofanya Rais Magufuli ya
kupambana na wazembe na wala rushwa,” alisema Kikwete.
Kikwete
alisema kazi hiyo anayofanya Dk Magufuli ni kubwa kwa kuwa inahusisha
kunyang’anya tonge watu na kusisistiza namna bora ya kumuunga mkono Rais
Magufuli, ni kulipa kodi na wakusanyaji wa mapato ya Serikali wawe
waaminifu.
“Ukitaka
kuongeza mapato bila kuziba mianya ya kuvuja kwa mapato ni sawa na
kutwanga maji kwenye kinu na anachofanya Rais ni kuumbua wote wanaokwepa
kodi,” alisema Kikwete.
*Kamati Kuu
Kikwete
ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, alisema hata katika kikao cha Kamati Kuu
ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho walichokaa juzi,
waliamua kumuunga mkono Rais Magufuli na kuwataka wanachama wote wa
chama hicho kufanya hivyo.
“Ni
pale tu mapato yatakapoongezeka, ndipo wajibu wa Serikali katika
kuhudumia wananchi utawezekana , tukimuunga mkono Rais wetu mzuri
ataweza na mapato yakiongezeka, maji yatapatikana, mapato yakiongezeka,
zahanati na hospitali zetu zitapata dawa za kutosha, mapato yakiongezeka
barabara za lami zitajengwa,” alisisitiza.
Kikwete
alisema akizungumzia kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza mapato ya
Serikali Kuu, hivyo hivyo inapaswa kutekelezwa katika halmashauri.
Alisema
katika Serikali Kuu, makusanyo yako nyuma ya asilimia 10 ya lengo,
lakini kwa juhudi za Rais Magufuli, hali inavyokwenda lengo hilo
litapitwa na Serikali itaanza kuzungumzia makusanyo ya matrilioni kwa
mwezi.
Hata
hivyo alisema juhudi hizo za Serikali Kuu hazionekani katika halmashauri
ambako ni kama hakuna kazi inayofanyika na hata pale kunapokuwa na
juhudi za kukusanya mapato, wakati mwingine yanaishia mikononi mwa
wajanja.
*Usafi
Kikwete
ambaye alifanya usafi katika soko ikiwemo kufagia, kukusanya na kuzoa
taka akiwa na mkewe, huku akikataa kuvaa vifaa vya kuzuia vumbi,
aliwataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi.
Alisema
uamuzi wa Rais Magufuli wa kutuma maadhimisho ya miaka 54 ya Uhuru
kuwataka wananchi wote wafanye usafi ni wa busara na si wa kukurupuka
kwa kuwa mwaka huu taifa lilikabiliwa na ugonjwa wa kipindupindu.
Kikwete
alisema tangu Mei mwaka huu mlipuko wa ugonjwa huo ulipoanza Dar es
Salaam, ulisambaa kwenye mikoa 19 na kuambukiza watu 10, 894 huku watu
109 wakifariki.
“Kipindupindu
si rehema ya Mungu ni uchafu na kinasababishwa na kula uchafu na
kinyesi huku mwenezaji mkubwa akiwa inzi. Ukijiepusha kula chakula
kichafu, utajiepusha na kipindupindu,” alisema Kikwete.
Aliwataka
wananchi wasisubiri kukumbushwa, bali wajenge tabia ya usafi na usafi
huo uanzie nyumbani na wananchi na viongozi wahakikishe maeneo mengine
ikiwemo sokoni, hospitalini na katika vituo vya mabasi kunakuwa safi na
kuhakikisha utamaduni wa usafi unakuwa sehemu ya maisha na si kusubiri
kukurupushwa.


No comments:
Post a Comment