Mraghbishi Kootu Tome (wa pili kushoto) akiwa na mtendaji wa
kijiji Rabie Lebuna (mwenye shati la njano) na Mwenyekiti wa Kijiji,
Kerry Dukonya (wa pili toka kulia).
Na Kisuma Mapunda,Loliondo
Sasa ni dhahiri waraghbishi wanatambua majukumu na haki zao ndani
ya jamii. Uelewa wao umewapa fursa ya kuchukua hatua na kusimamia kile
wanachoamini kwa manufaa ya wanajamii wanaowatumikia.
Watu hawa wamekuwa mhimili muhimu wa kuleta mabadiliko katika
maeneo wanayoishi. Lakini inapendeza zaidi kuona waraghbishi hao
wakijawa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi wao kwa kujitokeza
kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kama ilivyo kwenye Kijiji cha
Ololosokwani, kilichopo katika tarafa ya Loliondo, wilayani Ngorongoro,
mkoani Arusha.
Kijiji hiki kina jumla ya kaya 1,520 zinazoundwa na vitongoji
vinne vya kijiji, ambavyo ni Sero, Ololosokwani, Mairowa A na B. Baadhi
ya wanaounda kaya hizo ni pamoja na waraghbishi wanaofanya kazi na mradi
wa Chukua Hatua, akiwamo Kootu Tomu, mama wa watoto sita kutoka
kitongoji cha Mairowa.
Mraghbishi Kootu Tome (kushoto) akigawa nakala za Riwaya za Chukua
Hatua kwa baadhi wa wananchi wa kijiji cha Ololosokwani ikiwa kama
sehemu yake ya uraghbishi. (Picha na Kisuma Mapunda)
Tomu ni mmoja wa waraghbishi wa kwanza kuanza kufanya kazi na
mradi wa Chukua Hatua wakiwa na jukumu la kufuatilia ahadi za wagombea
wakati wa uchaguzi wa mwaka 2010. Ni katika uraghbishi huu wa
kufuatilia ahadi zilizokuwa zinatolewa na wagombea, ndipo alipojifunza
taratibu na kanuni za kuwa kiongozi bora.
Miaka mitano baadaye, alijitokeza katika kinyang’anyiro cha kuomba
kuchaguliwa na wanachama wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
kura ya ndani ya maoni. Na baada ya hapo alipata fursa ya kupeperusha
bendera ya chama chake na kuchaguliwa katika uchaguzi uliofanyika mwezi
Disemba mwaka 2014.
Mkurugenzi Mtendaji wa PALISEP, Roberth Kamakia,akielezea jambo
katika mkutano uliokutanisha waraghabishi toka mikoa ya Arusha ,Simiyu
na Shinyanga uliofanyika hivi karibuni
Akielezea jinsi ilivyokuwa Kootu Tomu anasema:
“Nilifahamu jukumu lililokuwa mbele yangu katika kusimamia haki
kwenye migogoro ya ardhi katika eneo letu. Hivyo, katika uchaguzi
uliopita wa serikali za mitaa niliomba ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mjumbe
wa kijiji kupitia CCM na nilichaguliwa. Sasa naweza kuwafikia wananchi
wengi zaidi hasa akinamama kupitia fursa hii ya uongozi niliyopata,”
Ndani ya halmashauri ya serikali ya kijiji cha Ololosokwani,
mraghbishi huyu amechaguliwa kuwa mmoja kati ya wajumbe 9 wanaounda
kamati ya elimu.
Akiwa kama mjumbe wa kamati hiyo, anafafanua majukumu yake:
“Moja ya jukumu la kamati yetu ni kusimamia upatikanaji wa ada kwa
wanafunzi. Kijiji chetu kinapata fedha kutoka idara ya wanyama pori,
ambazo ndiyo hutumika kulipia ada za watoto kwenye kijiji chetu.”
Katika kijiji cha Ololosokwani, kila mtoto anapata fursa ya kupata
elimu kwa kulipiwa gharama stahiki kuanzia ngazi ya shule ya msingi
hadi kiwango cha shahada ya uzamili.
Serikali ya kijiji hiki imejiwekea utaratibu wa kuhakikisha
walengwa wanapata huduma husika na kuhakikisha wanatoa taarifa za
kweli.
Akifafanua utaratibu huo, mwenyekiti wa kijiji cha Ololosokwani, Kerry Dukonya anasema:
“Jambo la kwanza ni mwanafunzi kutafuta shule na baada ya kupata
atatakiwa kuleta fomu na barua ya kukubaliwa kujiunga na shule husika
kama kielelezo. Barua hiyo ndio inayotoa maelezo ya ada na mahitaji
mengine ya shule. Ndipo hapo kamati inafuatilia na kuhakiki taarifa,
kabla ya kupitishwa na halmashauri ya serikali ya kijiji.”
Waraghbishi wamekuwa msaada mkubwa katika kutimiza majukumu ya
serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika harakati za kuhimiza wananchi
kutambua haki na majukumu yao katika kijiji. Na viongozi wa kijiji
wanakiri kwamba waraghbishi wamekuwa wakishawishi wananchi kuchukua
hatua mbalimbali, ikiwamo kuwawajibisha viongozi wazembe.
Akifafanua hali hiyo na jinsi viongozi wanavyojisikia iwapo
uraghbishi utagusia masilahi yao hasa linapokuja suala la kuwawajibisha,
mwenyekiti wa kijiji anasema:
“Sisi kama viongozi, tunamruhusu Kootu kwenda popote na akinamama
hawa wamekuwa mstari wa mbele kutukosoa na kutukumbusha majukumu yetu.
Hii ni njia mojawapo ya kuruhusu haki itendeke. Hivyo ni haki ya
wananchi kujua mapato na matumizi ya serikali yao ambayo sisi kama
viongozi tunayasimamia.”
Kama mwanamke ndani ya halmashauri ya serikali ya kijiji,
amepatiwa jukumu maalumu la kuhakikisha wanawake na wasichana
wanashiriki katika shughuli za maendeleo. Akifafanua jambo hilo,
mwenyekiti wa Ololosokwani, Kerry alisema:
“Tungependa kuona anakuwa kielelezo cha mwanaharakati mwanamke
kutokana na nafasi yake kama mjumbe wa halmashauri ya serikali ya
kijiji. Lakini pia wanawake wamekuwa ni kundi la pembezoni, ikiwamo
walemavu. Mraghbishi huyu atakuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wenzake
kutambua umuhimu wa elimu.”
Mraghbishi Tome, kwa kutumia mbinu za kiuraghbishi, anahakikisha
watoto wa kike wanakwenda shule. Katika hili, anaeleza anaeleza mikakati
yake:
“Kama mraghbishi, nimepata fursa ya kukutana na akinamama na
kuhakikisha watoto wa kike wanapata nafasi za kusoma. Lakini siku zote
nimekuwa nikiwataka kuwasiliana na walimu ili watambue changamoto
zinazowakabili watoto wao wa kike, hasa kwa wale ambao wapo mashuleni
tayari,”
Kwa upande wake, mtendaji wa kijiji Rabia Legula anasema:
“Ninapozungumzia mraghbishi, namaanisha wale wanaohamasisha
wananchi kudai haki zao za msingi, ikiwamo kuwawajibisha viongozi. Si
hivyo tu, waraghbishi wamekuwa mstari wa mbele kunisaidia masuala
yanayohusu wanawake. Kupitia ujuzi wao na kama wanawake waraghbishi
tunatoa kipaumbele kwa wanawake.”
Katika jamii ya kimasai ambayo bado wanawake hawajapata nafasi ya
kutosha, uwepo wa waraghbishi wanawake umekuwa chachu nzuri ya
kuwawezesha wenzao kuongea katika mikutano ya hadhara.
“Tunapenda waraghbishi waendelee kuhamasisha akinamama kuongelea
masuala yao katika mikutano ya vijiji. Kwa kutumia nafasi yangu ya
utendaji, nitahakikisha natoa fursa kwa waraghbishi hawa kuzungumza kwa
uwazi mambo ya wanawake.”
Kama mjumbe wa halmashauri ya serikali ya kijiji, mraghbishi
amekuwa na jukumu la kuhakikisha wananchi wanahudhuria mikutano ya
kijiji.
“Huwa nawahamasisha akinamama wenzangu kuhudhuria mikutano ya
kijiji kila tunapokutana kwenye vikundi vyetu vya ushirikiano,”
anasema.
Awamu ya pili ya mradi wa Chukua Hatua, unalenga kuwawezesha
waraghbishi wa zamani kufundisha waraghbishi wapya waliochaguliwa na
serikali za kijiji, kama anavyoelezea Mkurugenzi Mtendaji wa PALISEP,
Roberth Kamakia,
“Tuliwaandikia barua serikali za vijiji tukiwaomba watuchagulie
watu wanaofaa kuwa waraghbishi. Tuliwapa sifa za watu hao na mwongozo wa
jinsi ya kuwachagua.
Baada ya waraghbishi hao kuchaguliwa, waliandaliwa kwa ajili ya
mafunzo ya pamoja ikijumuisha wale wa zamani na wapya. Na baada ya hapo
waraghbishi wa zamani walikuwa na jukumu la kuwafundisha wenzao jinsi ya
kufanya uraghbishi.
Katika mafunzo hayo, walikumbushwa maana ya uraghbishi na sifa za
uraghbishi. Ndipo wale waraghbishi wa zamani, akiwamo Kootu walipopewa
jukumu la kufundisha wenzao kwa kutumia uzoefu waliopata wa uraghbishi.
Akielezea jinsi wao waraghbishi wa zamani wanalivyofundisha
waraghibishi wapya wanaotoka vitongoji vya Ololosokwani na Njoroi, Kootu
anasema:
“Tulikaa pamoja PALISEP na kuwafundisha waraghbishi wapya. Kwa
upande wangu, nilifundisha maana ya uraghbishi na kutoa maana ya mtu
anayeitwa mraghbishi Kazi yake ni kuwahamasisha wananchi. Mraghbishi
anatakiwa awe na sikio kubwa la kusikiliza, mdomo mdogo wa kuongelea na
macho makubwa ya kuangalia,” anasema.
Kootu si mraghbishi pekee aliye kwenye halmashauri ya serikali ya
Kijiji cha Ololosokwani, mraghbishi mwingine ni Noorkishili Naing’isa ni
mjumbe wa halmashauri na kamati ya fedha. Ni dhahiri waraghbishi
wanawake wameendelea kuwa chachu ya maendeleo kutokana na utendaji wao
mzuri kwenye serikali za kijiji. Hivyo ni jukumu letu sote kuhakikisha
harakati hizi za uraghbishi ndani ya halmashauri za vijiji vyetu
zinaungwa mkono.
No comments:
Post a Comment