Jumla
ya wanafunzi 503,914 kati ya 518,034 waliofaulu mtihani wa kumaliza
elimu ya msingi kwa kupata alama A, B na C, wamechaguliwa kujiunga
kidato cha kwanza katika shule za sekondari za Serikali katika awamu ya
kwanza. Idadi hiyo ni sawa na asilimia 97.3 ya wanafunzi waliofaulu na
wenye sifa ya kujiunga na kidato cha kwanza.
Hata
hivyo, wanafunzi 12,847 kati ya hao waliofaulu kutoka mikoa ya Dar es
Salaam, Dodoma na Mtwara, wameshindwa kujiunga na kidato cha kwanza
katika awamu ya kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.
Akitangaza
matokeo hayo jana Dar es Salaam, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tamisemi,
Selemani Jaffo alisema wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza kwa mwaka 2016 ni 503,914 kati yao, wasichana ni 255,843 sawa na
asilimia 99.2 na wavulana 248,071 sawa na asilimia 97.7.
Alisema
takwimu hizo zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza imeongezeka kwa
asilimia 0.7 ikilinganishwa na asilimia 97.23 ya wanafunzi
waliochaguliwa awamu ya kwanza kuingia kidato cha kwanza mwaka 2015.
“Wanafunzi
610 sawa na asilimia 61.2 ya wanafunzi 997 wenye ulemavu waliofanya
mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi wamefaulu na wote wamechaguliwa
kujiunga na shule za sekondari na ufaulu wao ni sawa na ongezeko la
asilimia 0.6 ikilinganishwa na ufaulu wa mwaka 2014,” alisema Jaffo.
“Naagiza
mikoa na halmashauri zenye wanafunzi hawa 12,847 ambao wamekosa nafasi
ya kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza kuhakikisha kuwa
wanakamilisha vyumba vya madarasa kabla ya Machi mwakani ili kuwezesha
wanafunzi hawa kujiunga na kidato cha kwanza,” alisema Jaffo.
Katika
hatua nyingine; Jaffo alisema Serikali imetenga Sh18.77 bilioni kwa
kila mwezi kuanzia mwezi huu hadi Juni 2016 kwa ajili ya kugharamia
uendeshaji wa shule za Serikali kuanzia ngazi ya msingi hadi kidato cha
nne ikiwa ni pamoja na chakula cha wanafunzi kwa shule za bweni na ada.
No comments:
Post a Comment